SIDO YAENDELEA KUWAWEZESHA WAJASIRIAMALI VIJANA

Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), linaendelea kutekeleza mpango wake wa kuwawezesha Wajasiriamali katika shughuli zao, ikiwa ni pamoja na uongezaji thamani wa mazao.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe ameyazungumza Bungeni Jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Bukene, Seleman Zedi aliyeuliza Je, kuna mpango gani wa kutoa mafunzo ya utaalam, mitaji, kuwaunganisha na masoko wajasiriamali wanaoongeza thamani ya mazao.?

Akijibu swali hilo, Kigahe amesema, “Mheshimiwa Spika, utekelezaji huo hufanywa kwa kutoa Mafunzo, ushauri, uwezeshaji upatikanaji wa Teknolojia za usindikaji wa mazao ya kilimo na uchakataji wa bidhaa mbalimbali. kuwawezesha Wajasiriamali kupata mitaji ambapo SIDO imekuwa ikitoa mikopo midogo.”

“Pia imekuwa ikiwaunganisha Wajasirimali wenye mahitaji ya mikopo mikubwa na Taasisi za kifedha ambazo Shirika limeingia nazo makubaliano, na kuwaunganisha Wajasiriamali kushiriki maonesho yanayoandaliwa na wadau mbalimbali kitaifa na kimataifa kwa lengo la kutangaza bidhaa na kupata soko la bidhaa zao.” amesema Kigahe.

Aidha, ameongeza kuwa Serikali kwa kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS), imekuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo kwa Wajasiriamali Wadogo na Kati wanaojihusisha na biashara ya kusindika bidhaa mbalimbali ikiwemo bidhaa za vyakula.

“katika utekelezaji wa mpango huo, mafunzo ambayo yamekuwa yakitolewa kwa kushirikiana na SIDO, utaratibu huo umesaidia si tu kusindika vyakula bali kupata teknolojia sahihi zinazosaidia kuzalisha bidhaa zenye viwango, mikopo, majengo na elimu ya biashara na masoko,” amesema Kigahe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *