SERIKALI YANDAA MKAKATI KULETA AHUENI YA GESI KWA WANANCHI WA KIPATO CHA CHINI

Na Gideon Gregory – Dodoma. 

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis amesema Serikali inaendelea na ukamilishaji wa taratibu za kuanzisha Mfuko wa Nishati safi ya kupikia, ili kuweka ruzuku itakayowawezesha Wananchi wa kipato cha chini kumudu bei ya gesi. 

Khamis ameyabainisha hayo leo Februari 12, 2025 Bungeni Jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Rungwe, Anton Mwantona aliyehoji ni lini Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Taasisi zinazohudumia watu wengi zinaweka mifumo ya majiko ya gesi ili kuokoa mazingira.

Amesema, “Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha uandaaji wa Kanuni ya Katazo la Matumizi ya Kuni na Mkaa kwa Taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kwa siku. Kanuni hizo zitajumuisha Taasisi za Umma na Binafsi.”

Ameongeza kuwa, katika kuhakikisha Taasisi zinazohudumia watu wengi zinaweka mifumo ya majiko ya gesi ili kuokoa mazingira, Serikali imetekeleza jitihada mbalimbali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini ikiwemo katazo la matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi za Umma na Binafsi zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya mia moja ambapo jumla ya Taasisi 551 zimeanza matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Serikali inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa nishati safi ya kupikia na  Kusaini  makubaliano  ya awali na wawekezaji mbalimbali ikiwemo makampuni ya gas kuhusu kutoa Ruzuku ya shilingi Bilioni 8.64 kwenye nishati safi ya kupikia ili kupunguza mzigo wa gharama kwa watumiaji wa nishati safi ambapo jumla ya majiko 452,455 yamepata ruzuku,” amesema Khamis.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *