Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amewataka wamiliki wa Shule binafsi na Shule za Umma kuhakikisha wanajenga mifumo imara ya ulinzi ikiwemo kufunga camera za uangalizi (CCTV) kwenye maeneo ya Shule na kwenye magari yanayobeba Wanafunzi, ili kuongeza usalama na uangalizi.
Bashungwa amesema hayo akiwa katika ziara Mkoani Mwanza ambapo amesema kwasasa Teknolojia inaruhusu kufunga kamera katika meneo ya shule na kwenye magari ya shule na kutokana na uwepo wa kamera hizo utasaidia kubaini changamoto zozote zile ambazo zinaweza kutokea pale mtoto anapokua shule au kwenye magari yanayowabeba wanafunzi hao.
![](https://jambofm.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/Screenshot_20250211-203134_Gmail.jpg)
Katika hatua nyingine Bashungwa pia amewaomba wazazi kutenga muda wa kufuatilia mienendo ya watoto wao pale wanapokua nyumbani ili kuweza kujua tabia zao na kujua namna ya kukabiliana nazo.
Aidha pia ameliagiza jeshi la polisi nchini kuyahakiki makampuni yanayotoa huduma za ulinzi katika taasisi mbalimbali za umma na binafsi ili huduma hizo zitolewe na makampuni yenye uwezo wa kumudu shughuli hizo.
![](https://jambofm.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/Screenshot_20250211-203103_Gmail.jpg)
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbroad Mutafungwa amesema hali ya ulinzi na usalama katika mkoa huo ni shwari na jeshi hilo litaendelea kuimarisha usalama dhidi ya vitendo vya kiuhalifu ambavyo vinaweza kutokea.
Nao baadhi ya Wazazi wa Wanafunzi waliokua wametekwa jijini Mwanza wamelishukuru jeshi la Polisi, Uongozi wa shule pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali kwa jitihada mbalimbali walizochukua hadi kufanikisha kuwanusuru Watoto wao.
![](https://jambofm.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/Screenshot_20250211-203202_Gmail.jpg)
Maagizo hayo yamekuja ikiwa ni siku chache tu toka tukio la utekaji wa watoto wawili wa Shule ya Blessing Modern litokee mkoani Mwanza na baadae watoto hao kupatikana wakiwa hai, waziri amefika shuleni hapo kuona maendeleo ya watoto kisha kutoa maelekezo ya Serikali.