NDEJEMBI AAGIZA UUNDWAJI WA KAMATI KUMALIZA MGOGORO WA ARDHI MWANZA

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi amemuagiza Kamishna wa Ardhi nchini, Mathew Mhonge kuunda mara moja kamati kwa ajili ya kushughulikia mgogoro wa ardhi wa kiwanja namba 01, Kitalu R kilichopo mtaa wa Barabara ya Nyerere

Ndejembi ametoa agizo hilo leo wakati alipotembelea katika kiwanjani hicho kilichopo jijini Mwanza ambapo amesikiliza malalamiko ya pande zote mbili ambazo ni mmiliki Z.E.K Ladhan Ltd na Halmashauri ya jiji la Mwanza.

Waziri huyo ameagiza hadi kufikia ijumaa ya wiki hii (februari 14) kamati hiyo iwe tayari imepatikana ikihusisha wajumbe kutoka Wizara yake na Mkoa wa Mwanza aidha ifanye kazi ya kupitia nyaraka kwa siku saba kuanzia februari 17, 2025 na itoe mapendekezo ya nani mmiliki halali na nini kifanyike.

Katika hatua nyingine Ndejembi pia ametoa wito kwa jamii kuendelea kufuata sheria wakati wanapotaka kumiliki ardhi ili kujiepusha na migogoro na kwa upande wa watumishi wa serikali (Sekta ya Ardhi) amewasihi kuendelea kufanya kazi kwa kufuata maadili ya utumishi wao kwa mujibu wa kanuni na sheria.

Akijibu hoja ya mwananchi mmoja aliyetaka kufahamu hatma ya wananchi waliovamia eneo la Mamlaka ya Viwanja vya ndege katika Manispaa ya Ilemela na kuzuiwa kuviendeleza, Ndejembi amesema serikali inashughulikia suala hilo na siku za usoni itaketi nao kuzungumza na kumaliza mgogoro huo

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amemshukuru Waziri wa Ardhi kwa utendaji wake unaolenga kumaliza migogoro ya ardhi nchini hususani mkoani humo na amemuahidi kushiriki vema kwenye uundaji wa kamati hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *