Aliyekua Kada na Mwanachama wa CCM, Mchungaji Godfrey Malisa leo Februari 10, 2025, ametangazwa kuvuliwa uanachama wa chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, kwa tuhuma za kukiuka Katiba na maadili ya Chama hicho.
Mchungaji Malisa, ambaye awali amewahi kugombea nafasi mbalimbali ikiwemo urais, Uspika na Ubunge, alitangaza kujiunga na CCM mwaka 2021 akiwa miongoni mwa Wanachama tisa waliochukua fomu kugombea uenyekiti wa Chama hicho mwaka 2022.
Kuvuliwa Uanachama wa Malisa kunasemekana kuwa kunatokana na kauli alizozitoa za kupinga uamuzi wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa uliokaa Januari 19, 2025 na kupitishwa kwa wagombea wake (Rais Samia Suluhu Hassan (Tanzania Bara) na Dk Hussein Mwinyi- Zanzibar) kumekiuka Katiba ya CCM.
Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Merce Mollel mbele ya waandishi wa habari leo amesema uamuzi huo umefikiwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM ya mkoa.