Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
MADIWANI wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, wamepitisha Rasimu ya Mpango wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026 sh.bilioni 44.9,kwenye kikao maalumu cha baraza la bajeti kilichoketi leo tarehe 30 january 2025 katika ukumbi wa mikutano wa halimashauri hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ngassa Mboje,amesema rasimu ya bajeti hiyo sh.bilioni 44.9,imegusa maisha ya wananchi na ndiyo dira ya Halmashauri.
“Nawauliza Madiwani,Rasimu hii ya Mpango wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 ya sh.bilioni 44.9 katika Halmashauri yetu ya wilaya ya Shinyanga je? mmeipitisha…”aliuliza Mboje.
Nao Madiwani wa Halmashauri hiyo,walijibu kuwa wameipitisha, ambayo pia ndiyo itakuwa dira ya halmashauri katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Ibrahimu Makana, amewapongeza madiwani hao kwa kujadili Bajeti hiyo kwa umakini pamoja na kuipitisha,huku akiagiza menejimenti ya halmashauri, kwamba mapendekezo ambayo yametolewa na madiwani juu ya bajeti hiyo yaingizwe kwenye mfumo na kutekelezwa.
Ameagiza pia kwa Watumishi wa Afya pamoja na Walimu, ambao wanafanya kazi kwa kujitolea kwa kufanya ajira za muda, kwamba nao malipo yao yaingizwe kwenye Bajeti hiyo.
Aidha,Madiwani hao pia walijadili na kupitisha Bajeti za kwenye Taasisi katika mwaka huo wa fedha 2025/2026, ikiwamo SHUWASA sh.milioni 825, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji.
Bajeti nyingine ni ya Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA)sh.bilioni 2.4 kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya barabara.
Bajeti nyingine ni ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS),ambao watajenga barabara ya Oldshinyanga-Salawe kilomita 65 sh.milioni 773, na barabara ya Didia hadi Ntobo kilomita 8.4 sh.milioni 140.