Siwezi kukubali nchi au bandari kuuzwa

Watanzania wametakiwa kuheshimu sheria na kuwa makini dhidi ya propaganda za kisiasa wakati wakiendesha majadiliano kuhusiana na mkataba ya utekelezaji wa makubaliano ya uendeshaji wa maeneo ya bandari nchini kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kupitia Kampuni ya DP World.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mh. Patrobas Katambi wakati akizungunza wananchi katika Tamasha la Sukuma Festival lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Nhelegani Julai 9,2023 na kufafanua kwamba hakuna fedha iliyoliwa ili mkataba huo utekelezwe.

Aidha Katambi amefafanua kuwa hakuna mtu au kiongozi yeyote anayeweza kuruhusu nchi kuuzwa kama ambavyo imekuwa ikielezwa na wanaopotosha kuhusiana na mkataba huo na kuhoji ikiwa nchi itauzwa wananchi watakwenda wapi?

“Hivi kama tukiuza nchi yetu tunakwenda wapi,tunataka turudi utumwani?Hakuna kitu kama hicho,maelezo yanakuwa yanaelezwa na kila mtu anavyojua kwasababu changamoto kubwa ya kwanza kwa mwanasheria yeyote ni uwezo wa kusoma sheria,kujua sheria ilivyo,kuielewa na kuitumia” amesema Mh. Katambi.

Aidha amefafanua kwamba mkataba wowote wa kisheria ulio sahihi kwa mujibu wa sheria ya mikataba sura namba 345 lazima kuwe na mlango wa kuingilia na kutokea tofauti na inavyoelezwa kwamba hakuna ukomo katika mkataba wa bandari na kwamba hata yeye hawezi kukubali uwepo wa mikataba inayouza taifa au bandari zetu.

Mkataba huo wenye ibara 31 ulisainiwa Oktoba 25, mwaka jana kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai ili kuendeleza na kuboresha uendeshaji wa miundombinu ya kimkakati ya bandari pamoja na maeneo maalumu ya kiuchumi, maegesho ya utunzaji mizigo na maeneo ya kanda za kibiashara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *