Maajabu bado yanaendelea, ingawa hili ni la kitambo sana lakini litakushangaza. Ni kuhusu Mwanasayansi na mtafiti wa nchini Romania, Nicole Minovici ambaye alitaka kukitafiti kifo kwa kufanya uchunguzi kujua mtu akifa hujisikiaje.
Minovici alienda mbali zaidi na kufanya majaribio kadhaa ya kujiua ili apate jibu halisi yeye mwenyewe na si kusimuliwa kwani siku moja alijinyonga mbele ya wasaidizi wake lakini aliwataka wafuatilie hatua zote anazopitia na wakiona anakaribia kufa wamuokoe haraka.
Jaribio la kwanza lilikuwa ni kujitia kitanzi kupitia kamba iliyofungwa darini, anasema katika jaribio hilo uso wake mara moja ulibadilika kuwa mwekundu na macho yake yalimtoka na uoni kufifia na pia anadai alisikia mlio masikioni mwake.
Hata hivyo, anadai kuwa chamoto alikiona kwani hali zote hizo alizisikia kwa muda wa sekunda sita tu na baada ya hapo akaanza kupiga kelele kuomba msaada ndipo Wafanyakazi wake wakaenda haraka kumtoa na ndipo akasema ni kweli amejifunza kitu, lakini bado hajaelewa vizuri.
Alirudia kufanya majaribio mengine kama hayo mara 12, lakini moja ya jaribio lilipelekea kuumia shingo na kulazwa Hospitali kwa kutoweza kula chochote kwa majuma manne akisema hilo hakujali bali shauku yake ya kujua nini mtu hupitia wakati wa kunyongwa ilikuwa imetimia.
Hata hivyo, Mwamba huyo (Nicole Minovici) aliaga dunia kutokana na matatizo ya koo na wengi wanaamini ni lile tukio la kujinyonga ingawa wengine wanapinga wakisema ni maradhi.
Nicolae Minovici alizaliwa Oktoba 23, 1868 na alifariki Juni 26, 1941, yeye kitaaluma alikuwa ni Mwanasayansi mchunguzi wa Kiromania na mtaalamu wa uhalifu ambaye alihudumu kama mkuu wa huduma ya anthropometric.
Anajulikana kwa tafiti zake za kuchunguza uhusiano kati ya kuchora tattoo na tabia ya uhalifu, pamoja na utafiti wake kuhusu kunyongwa na athari zake za kisaikolojia kwenye mwili wa binadamu.