WAVIPATIA VICHAKA MAJINA KUPATA UHALALI WA KUJISAIDIA, WAPEWA SAA 24 KUJENGA VYOO

Saada Almasi – Simiyu.

Mtendaji wa Kata ya Somanda Wilayani Bariadi Mkoani Simiyu, Daniel Gesase amepewa saa 24 na Wakazi wa kata hiyo kuhakikisha wanajenga vyoo huku akiwataka kuacha tabia ya kuhalalisha utumiaji na kuvipa vichaka majina ili kujisaidi kulingana na hadhi ya mtu.

Hatua hiyo imekuja baada ya visa sita vya kipindupindu kuripotiwa katika kata hiyo ndani ya miezi miwili iliyopita, huku ukosefu wa vyoo ukitajwa kuwa ni moja ya sababu.

Akizungumza katika kikao cha nzengo kilichojumuisha wakazi wa mtaa wa Nyamimbi, Gesase amesema kumekuwa na utaratibu mbovu wa kujisaidia katika mashamba na vichakani huku vichaka hivyo vikipewa majina kulingana na baba, mama au mkwe ambaye hukitumia kujisaidia.

“Mnaingia kujisaidia mashambani na kwenye vichaka mmefika mbali zaidi na kuvitambua kabisa hiki ni kichaka cha mama cha baba mara mkwe hivi hamuoni aibu,mtu yuko radhi ajenge nyumba ya milioni kumi au ishirini lakini asijenge choo cha milioni moja,” alisema Gesase.

Gesase amesema kwa yeyote ambaye hana mpango wa kujenga choo katika nyumba yake kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani sambamba na faini ya kiasi cha shilingi elfu 50.

“tulishazungumza sana tangu janga hili litufikie lakini bado hamuelewi na inaonekana hamko tayari mmezowea kuishi bila vyoo kwani kwa kipindi ambacho tumekuwa tukisema hadi sasa wote mngekuwa na vyoo sasa hatuwezi kuwachapa viboko tutakukamata sheria ichukue mkondo wake,” alihimiza Gesase.

Kwa upande wake mhudumu wa afya ngazi ya jamii, Rebecca Balaja amesema desturi na mazoea mabovu ya mtindo wa Maisha ndio unaoleta ugumu katika suala la kutokomeza ugonjwa huo kwani pindi wanapofikiwa na wahudumu hao hukimbilia kujificha shambani.“

“mama anamtawaza mtoto hanawi na sabuni yeye mwenyewe anajisaidia porini kipindi hiki cha mvua kile kinyesi kinabebwa na maji kisha maji yale yanatuama wanayachukua tena kwenda kupikia na wakati mwingine wakiona tumepiga hodi wanakimbilia mashambani wanasema huyo nae amekuja na habari zake za choo,” alibainisha Rebecca.

Naye mjumbe wa nyumba kumi, Maria Alphonce amewataka wakazi hao kutumia nyenzo walizonazo kama miti kuhakikisha katika kipindi ambacho wanakusanya nguvu ya kujenge vyoo vya kudumu wawe na vyoo ambavyo watajistiri wao na familia zao.

“Msije kusema tumelazimishwa kujenga vyoo vya kisasa vyenye gharama kubwa isipokuwa kwa kipindi ambacho mnajipanga kuna miti maeneo yenu tumieni jengeni vyoo ili pale mnapopata uwezo muwe tayari mmeshakuwa na mahali pa kutumia kisha mkarabati vyoo vyenu,” alisema Mjumbe Maria.

Kufuatia agizo hilo baadhi ya wakazi wa mtaa huo wameiomba serikali kuwapatia muda wa wiki mbili ili kukamilisha zoezi la ujenzi wa vyoo hivyo sambamba na kuipitisha adhabu shilingi elfu 50 na mahakama kewa atakaye puuza agizo hilo

Licha ya jitihada ambazo Serikali ya Mkoa huo imekuwa ikizifanya tangu kutangazwa kwa janga la kipindupindu mwaka 2023, bado jamii imeonekana kutokutilia maanani suala la usafi wa mazingira, ikiwa ni pamoja na kujenga vyoo bora.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *