MUTAFUNGWA AKEMEA WIZI MAZAO YA UVUVI, 115 WADAKWA

Wananchi wanaoishi visiwani na pembezoni mwa ziwa Viktoria wameombwa kujiepusha na viendo vya uvuvi haramu huku pia wakijiepusha na wizi wa mazao ya uvuvi kwani ni jambo ambalo lipo kinyume na sheria.

Hayo yameelezwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa ambae amesema katika misako na doria zilizofanyika kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 15 hadi 20 Januari 2025 katika mialo na visiwa vya Yozu, Nyamango, Soswa na maeneo ya Kanyala na Mbugani kata ya Bulyaheke, Halmashauri ya Buchosa kwenye Ziwa Victoria.

Jeshi la polisi mkoa wa Mwanza lilifanikia kukamata watuhumiwa 115, wa makosa mbalimbali ya jinai ikiwemo wizi, uvuvi haramu na kuishi nchini bila kibali, ambapo 42 walikamatwa kwa tuhuma za wizi wa samaki ziwani (Uhengaji), watuhumiwa 19 kwa tuhuma za kuishi nchini bila kibali, watuhumiwa 12 kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya kihalifu.

Wengine ni watuhumiwa watatu kwa kupatikana na nyavu haramu aina ya Timba, watuhumiwa 2 kwa kupatikana na Bhangi, watuhumiwa 16 kwa kujipatia kipato kwa njia ya ukahaba, watuhumiwa 3 kwa kukiuka masharti ya leseni ya biashara, watuhumiwa 12 kwa tuhuma za kucheza kamari, watuhumiwa 4 kwa kujeruhi, mtuhumiwa 1 kwa kupatikana na pombe ya moshi na mtuhumiwa 1 kwa tuhuma ya kumtaja mtu mchawi.

Katika hatua nyingine jeshi hilo pia limefanikiwa kukamata vielelezo mbalimbali ikiwemo mitumbwi 6 isiyokuwa na namba za usajili ambayo inatumika kufanya wizi wa mazao ya uvuvi, mashine moja ya kuendeshea Boti, nyavu haramu vipande 1,500 aina ya timba (Mono filaments), Bhangi kilogramu 5na pombe haramu ya moshi lita 30.

Sambamba na hayo Jeshi la polisi linaendelea na hatua mbalimbali za kiuchunguzi dhidi ya uhalifu na wahalifu na mara zitakapokamilika, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa wote ikiwemo kuwafikisha mahakamani.

Miongoni mwa watuhumiwa hao 115, watuhumiwa 31 wamefikishwa mahakamani na 11 wamehukumiwa kwenda jela miezi 12 baada ya kupatikana na hatia ya kujihusisha na ukahaba na watuhumiwa 20 kesi zao zinaendelea na zipo katika hatua mbalimbali, watuhumiwa wengine 81 watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *