Kesi ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Wilbroad Slaa (76), imesikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam hii leo Januari 17, 2025 ambapo ataendelea kusalia Mahabusu jadi Januari 23, 2025 kwa kukosa dhamana.
Dkt. Slaa ambaye anakabiliwa na shitaka la kusambaza taarifa za uongo katika mtandao wa X, kwa mara ya kwanza alifikishwa Mahakamani hapo Januari 10, 2025 akikabiliwa na kesi ya jinai namba 993 ya mwaka 2025.
Aidha, Januari 13, 2025 Dkt. Slaa pia alitarajiwa kufika Mahakamani hapo kwa ajili ya kujua hatma ya dhamana yake baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha kiapo cha kuzuia dhamana.
Wakili wa Serikali, Issa tawabu alisema kesi hiyo imeitishwa kwa ajili ya mjadala wa dhamana, lakini mtuhumiwa hakufika mahakamani hali ambayo ilizua vita nikuvute ya kisheria.
Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki aliahirisha kesi hiyo hadi leo Januari 17, 2025 na Mtuhumiwa anadaiwa kutenda kosa hilo chini ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.