Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), kwa kushirikiana na Bodi ya Filamu Tanzania, wametangaza rasmi ujio wa Tuzo za Wachekeshaji Tanzania, zitakazofanyika Februari 14, 2025, katika ukumbi wa The Super Dome Masaki.
Katibu Mtendaji wa BASATA, Dkt. Kedmon Mapana, akizungumza na wasanii, alisema kuwa kupitia serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi dhabiti wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, tuzo hizi zinalenga kutambua na kuonyesha thamani na mchango mkubwa wa wachekeshaji katika kukuza sekta ya sanaa nchini.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Dkt. Gervas Kasiga, alisisitiza kuwa tuzo hizi ni tunu muhimu kwa taifa, kwani wachekeshaji wana mchango mkubwa wa kupeperusha bendera ya Tanzania na kuendeleza utamaduni wetu kwenye majukwaa ya kimataifa.
Vipengele mbalimbali vya tuzo, ikiwemo kipengele cha Comedian of the Month, vitatangazwa rasmi katika mkutano na waandishi wa habari unaotarajiwa kufanyika mapema Februari. Wito umetolewa kwa wadau na wasanii kuzitangaza tuzo hizi kwa ubunifu na weledi ili kuzalisha hamasa na kuungwa mkono na watanzania wote.
Hii ni hatua muhimu katika kutambua na kuenzi juhudi za wachekeshaji katika tasnia ya sanaa na burudani nchini.