BIBI WA MIAKA ZAIDI YA 60 ALIYEACHIWA WAJUKUU MAPACHA AOMBA MSAADA……

NA William Bundala – KAHAMA

Bibi mwenye miaka zaidi ya 60 aliyefahamika kwa jina la Kashindye Mhoja mkazi wa Kata ya Mwendakulima Manispaa ya  Kahama Mkoani Shinynga ameiomba serikali na wadau mbalimbali kumsaidia kuwalea Watoto mapacha walioachwa baada ya mama yao kufariki kwa tatizo la upungufu wa damu.

Akizungumza na Jambo FM iliyomtembelea nyumbani kwake bibi Huyo amesema kuwa Baba wa Watoto hao hajulikani alipo kwani alitoweka mara tu baada ya mazishi na kwamba kwa sasa Watoto wanahitaji maziwa, Mavazi na sehemu ya kulala kwani hawana godoro na wanalazimika kulala kwenye mifuko ya Sandarusi.

“Mwanangu alipojifungua alipungukiwa damu ghafla baada ya wiki akafariki ghafla, Tukaenda kuzika ushetu tulipomaliza kuzika tu baba wa watoto alitoroka hadi sasa hapatikani kwenye simu na mimi hapa hali yangu ni mbaya sana sina uwezo wowote watoto hawa wanashida ya maziwa, Nguo hata godoro sina tunalala chini kwenye mifuko ya sandarusi” Alisema bibi huyo.

Sambamba na hayo Bibi Kashindye ameongeza kuwa kutokana na ukosefu wa maziwa analazimika kuwakorogea Watoto hao uji mwepesi sana wa unga wa kawaida ili wapate chochote na kwamba hali hiyo inasababisha afya zao kuanza kuzolota.

“Yaani nakosa pesa ya kununua maziwa ya kopo ninachofanya ni kukoroga uji mwepesi wa mahindi ili niwanyweshe lakini kadri siku zinavyoenda afya zao zinazidi kuzorota na sina jinsi mana sina uwezo kabisa naomba msaada niwalee wajukuu zangu hawa” Ameongeza bibi huyo.

Naye Jirani wa bibi huyo Selina Alphonce amesema kuwa hali ya Watoto hao ni mbaya na kwamba familia hiyo inahitaji sana msaada wa Chakula huku afisa maendeleo wa kata ya Mwendakulima Catherine Phales akisema kuwa tangu wazaliwe septemba 11 watoto hao waliishi kwa misaada ya nguo na maziwa kupitia vikundi mbalimbali na kutoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kuwashika mkono.

“Kiukweli hawa Watoto mapacha wanateseka sanaa,huyu Jirani yangu ni mzee na hana kazi inakuwa ngumu kuwatunza hawa Watoto niombe mumpe msaada mana wanamwelemea matunzo” Amesema Selina “Yani hawa Watoto tangu mama yao amefariki ilibidi niombe vikundi mbalibali hapa katani wanisaidie tukanunua maziwa na nguo za kuanzia na wengine wakaleta nguo mbalimbali kiukweli hali ya huyu bibi ni mbaya” Amesema Catherine.

Akiongea kwa njia ya Simu Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Kahama Ndg. Robert Kwela ameiambia Jambo FM kuwa ofisi yake ina taarifa ya Watoto hao na kwamba pale wanapokuwa na matatizo wanasaidiwa na kwamba kwasasa wanasaidiwa sana na jamii kwakuwa bado ni wadogo hawajafikia hatua ya kwenda shule na kwamba idara yake inawasaidia Watoto wengi wenye matatizo kama hayo.

“Ni kweli taarifa za Watoto hao zimefika ofisini kwangu  na kila wanapohitaji msaada tunajihadi kuwafikia japo kwa sasa bado wadogo misaada mingi inatoka kwa wanajamii kwakuwa bado hawajaanza masomo” – Amesema Kwela.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *