HEKARI ZAIDI YA 20 ZA BANGI ZATEKEZWA KWA MOTO TARIME….

Adam Msafiri. Tarime – Mara.

ZAIDI ya hekari 20 za mashamba ya bangi yameteketezwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama wilayani Tarime mkoani Mara na watu watano wakishikiliwa na Polisi kwa mahojiano zaidi.

Akizungumza na Jambo FM Januari 10,2024, Bw.Dezdel Tumbu Mwakilishi wa Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), ameiambia Jambo FM kuwa Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wamefanya msako wa siku 3 mfululizo ndani ya wilaya ya Tarime na kufanikiwa kubaini mashamba hayo ya bangi katika kijiji cha Matongo.

‘Tulikua na Oparesheni ya kumaliza tatizo la bangi kwenye mkoa wetu huu wa Mara,kama mnavyofahamu mkoa wa Mara umekithiri na kilimo cha mazao haramu ya bangi,kwahiyo tulikusanya taarifa kwa kushirikiana na wenzetu wa Jehi la Polisi na tukafanikisha kufanya Oparesheni,hawa wakulima wa bangi wanafanya kilimo hiki kwenye maeneo ya kujificha kisha wanazungushia mazao halali’” Amesema Bw. Tumbu ambaye pia ni Afisa Elimu kutoka DCEA Kanda ya Ziwa.

Aidha amewataka wakazi wa eneo hilo na maeneo mengine kote nchini,kuacha kabisa kilimo cha bangi,kuuza ama kutumia dawa hizo za kulevya,huku akitahadharisha kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sharia.

Aidha Afisa huyo ameeleza kuwa”Katika oparesheni hii takribani zaidi ya hekari 20 zimeteketezwa na watuhumiwa kadhaa wanashikiliwa kwa ajili ya mahojiano,Tuendelee kuwasihi wananchi kutafuta kilimo halali na waachanae na kilimo cha dawa za kulevya”

Naye Mkuu wa wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele ametoa rai kwa wakazi wa wilaya hiyo,kutumia fursa ya uwepo wa ardhi yenye rutuba kujielekeza katika kilimo cha mazao halali kuliko kujiiingiza kwenye uhalifu wa kilimo cha bangi.

‘’Maeneo mengi ya wilaya ya Tarime wanajihusisha na kilimo cha bangi lakini tumeendelea kudhibiti kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya,kilimo hiki hakikubaliki,wilaya hii tunalima alizeti,ndizi,kahawa,tunalima mahindi hivyo niwatake wananchi waendelee kulima mazao hayo’’. Amesema Mkuu wa wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *