WAWILI WANAODHANIWA KUWA MAJAMBAZI WAUWAWA MWANZA….

Watu wawili wanaodhaniwa kua ni majambazi wameuawa na askari wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza walipovamia na kutaka kupora kwenye nyumba ya Mfanyabiashara mmoja anaefahamika kwa jina la Flora Sungura.

kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa tukio hilo lilitokea siku ya tarehe 09.01.2025 majira ya saa mbili na dakika arobaini na tano usiku (20:45Hrs) huko katika mtaa wa Kabambo, kata ya Kiseke, wilaya ya Ilemela Mkoa wa Mwanza, ambapo watu hao wawili wa jinsia ya kiume wanaodhaniwa kuwa ni majambazi waliokuwa wamevalia mavazi ya kike ambayo ni gauni na vilemba wakiwa na bunduki aina ya Shortgun moja iliyotengenezwa kienyeji ikiwa na risasi mbili na mapanga mawili walivamia nyumba ya mfanyabiasha aitwaye Flora Sungura Abdallah miaka 42, wakati ambapo mfanyabiashara huyo anafunguliwa geti akitoka kwenye shughuli zake za kibiashara.

Baada ya wezi hao kuingia ndani ya nyumba hiyo wakazi wa eneo hilo walianza kupiga kelele za kuomba msaada na taarifa hizo ziliwafikia askari wa Jeshi la polisi waliokuwa doria katika eneo hilo na askari hao walipofika katika eneo hilo waliwataka watu hao kujisalimisha kwa hiari lakini walikaidi amri hiyo na kutaka kuwadhuru wakazi wa nyumba hiyo pamoja na askari na baada ya kukaidi amri hiyo askari wa Jeshi la polisi walifyatua risasi na kuwaua watu wawili ambao mmoja alishika bunduki na mwingine akiwa na panga.

Katika tukio hilo silaha aina ya Shortgun moja, mapanga mawili na begi la mgongoni likiwa na nguo suruali, shati, bisibisi na viatu vimepatikana kwenye eneo la tukio huku watu wawili wa jinsia ya kiume ambao walikuwa ni washiriki katika tukio hilo walifanikiwa kutoroka kwa kutumia usafiri wa pikipiki ambayo namba za usajiri hazijafahamika na hawakufanikiwa kuondoka na mali yoyote.

Msako mkali wa kuwatafuta watu hao waliokimbia na watu wengine ambao walipanga na kuratibu tukio hilo la kihalifu unaendelea ili waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria. Chanzo cha tukio hili ni kujipatia mali kwa njia isiyo halali. 

Katika hatua nyingine Mutafungwa amesema mpaka sasa miili ya watu hao wawili haijatambuliwa na imehifadhiwa katika hospital ya rufaa Bugando ikisubiri utaratibu wa utambuzi na uchunguzi wa kitaalamu (Post mortem) huku jeshi hilo likiendelea kufanya msakao mkali ili kuwatafuta watu hao waliokimbia na watu wengine ambao waliratibu tukio hilo.

Aidha Jeshi la Polisi katika mkoa wa Mwanza linatoa onyo kwa baadhi ya watu wanaopenda kutafuta riziki zao kwa kufanya vitendo vya kihalifu yakiwemo matukio ya ujambazi, uvunjaji na matukio mengine yasiyo halali, kutambua kuwa mkoa wa Mwanza sio sehemu salama kwao kufanyia matukio hayo na pia Polisi imewaomba wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la polisi katika kuwafichua wahalifu na uhalifu na kuwakumbusha Wafanyabiashara wenye uwezo kuweka CCTV Camera katika maeneo yao ya biashara na majumbani ili kurahisisha jitihada za Jeshi la polisi za kuwabaini na kuwadhibiti wahalifu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *