Mkuu wa mkoa wa Simiyu Kenani Laban Kihongosi amemuagiza mkurugenzi mtendaji wa wilaya ya Bariadi, Khalid Mbwana kumhamisha Afisa Mtendaji wa kata ya Igegu pamoja na Afisa Afya wa kata hiyo kwa kushindwa kusimamia ujenzi wa choo cha soko la Igegu.
RC Kihongosi amechukua hatua hiyo akiwa kwenye ziara yake ya kikazi wilaya ya Bariadi ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi baada ya kufika katika kata hiyo wananchi walifikisha kero yao ya ukosefu wa choo katika soko hilo hali inayohatarisha afya na maisha yao kutokana na magonjwa mbalimbali ya kuambukiza kama kipindupindu.
“Nimekuwa nikitoa maagizo hayatekelezeki sasa nakuagiza mkurugenzi hapa leta mtu mwingine wa afya na mtendaji leo tupate mtu mwingine atakaye simamia ujenzi wa choo tunapambana na kipindupindu tuokoe watu halafu soko halina choo” – RC Kihongosi.
Sambamba na hilo, kihongosi amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuachana na visingizio kwamba maji ya kunywa yakitibiwa kwa dawa yanakosa ladha na zaidi kupunguza nguvu za kiume jambo ambalo si kweli.
“watu mnasema maji yanayowekewa madawa yanapunguza nguvu za kiume hayo mnasema nyie siyo sisi maana serikali haiwezi ikaua wananchi wake tunakunywa dawa na malaria na magonjwa mengine
mbona hamuogopi?”- RC Kihongosi.
Aidha kihongosi amewataka wananchi kusafisha mazingira pamoja na kujenga vyoo na kuvitumia ipasavyo huku akiwaonya juu ya suala la kutochangia choo na mkwe na hatimaje kwenda maporini waache mara moja.
“We unajenga choo halafu unakimbilia porini kisa mkwe yupo huwezi kuchangia naye kweli? wengine mnashangaza unabeba jiwe unakwenda nalo hivi mna roho ngumu kiasi gani” – ameongeza Kihongosi