Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kituo cha Crown FM kinachomilikiwa na Alikiba kimesema kuwa Alikiba ametangazwa mshindi kwa kupewa tuzo ya heshima 2024 na mtandao wa NXT Honors kutoka nchini Nigeria na kumfanya kuwa mtu wa kwanza asiye Mnigeria kupokea heshima hii.
AliKiba ametajwa kama msanii mwenye mafanikio akiwa na zaidi ya miongo miwili ya mafanikio, Alikiba amejidhihirisha kama mwanzilishi wa miondoko ya Bongo Flava. Uwezo wake wa kuchanganya midundo ya jadi ya Kiswahili na sauti za kisasa umebadilisha muziki wa Afrika Mashariki na kumweka kama balozi wa kimataifa wa utamaduni wa Tanzania, akiwa na nyimbo zisizopitwa na wakati ambazo zimegusa vizazi mbalimbali. Alikiba anaendelea kuhamasisha mashabiki kote barani Afrika na duniani.
Akizungumzia tuzo hiyo, Saliu Momoh, Mkurugenzi Mtendaji wa NXT Honors, alimpongeza Alikiba kwa mchango wake:
“Mchango wa Alikiba katika muziki wa Afrika unazidi nyimbo zake. Amekuwa nguvu ya kiutamaduni, akiziba pengo kati ya bara lote la Afrika huku akibaki mwaminifu kwa mizizi yake. Ni haki tumtambue kwa urithi wake kwa heshima yetu ya juu kabisa.”
Mwaka 2023, Tuzo ya Heshima ya Maisha ilitolewa kwa mtayarishaji wa muziki wa Nigeria, Don Jazzy kwa mchango wake katika muziki wa Afrobeats. Kutambuliwa kwa Alikiba ni hatua muhimu, kwani NXT Honors inaendelea kusherehekea vipaji tofauti vinavyounda simulizi la kiutamaduni la Afrika.
NXT Honors 2024 itatangaza orodha kamili ya washindi katika muziki, filamu, mitindo, na ubunifu baadaye mwezi huu.
Contact Us
P. O. BOX 71, Shinyanga, Tanzania
+255 766 408 253
info@jambofm.co.tz