VYANDARUA ZAIDI YA MILIONI MOJA NA NUSU VYENYE DAWA KUSAMBAZWA SHINYANGA….

NA EUNICE KANUMBA –SHINYANGA 

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI, wameanzisha kampeni ya ugawaji wa vyandarua vyenye dawa ili kukabiliana na ugonjwa wa maralia ambao umekuwa ukipoteza maisha ya Watanzania wengi.

Hayo yamebainishwa leo Januari 6,2025 na Afisa Mwandamizi kutoka Wizara ya Afya Peter Gitanya kupitia mpango wa Taifa wa kudhibiti Malaria (NMCP),kwenye kikao kazi na waandishi wa habari wa mkoa wa shinyanga, kuhusina na  kampeni ya ugawaji wa nyandarua vyenye dawa kwa wananchi.

Amesema serikali kupitia mpango wake wa kudhibiti malaria nchini, wameanzisha kampeni ya ugawaji wa vyandarua vyenye dawa bure kwa wananchi kwa kupita kila Kaya, ili kupambana na ugonjwa wa malaria na kuutokomeza kabisa ifikapo 2030 huku akianisha kuwa kwa Mkoa wa Shinyanga vitasambazwa vyandarua vyenye dawa milioni 1.5 bure na Kaya zote zitafikiwa.

“Tupo katika zoezi la uhandikishaji kaya kwa kaya na kila chandarua kimoja watapewa watu wawili wawili kwa kila kaya” amesema Gitanya 

Amesisitiza kwamba, kwa kaya ambayo haitaandikishwa haitaweza kupewa chandarua,huku akiwasihi wananchi  washiriki zoezi hilo kikamilifu, ambapo maafisa watakuwa wakipita kwenye Kaya zao kuchukua taarifa, pamoja na kuwapatia kadi maalumu kwa ajili ya kuja kupewa chandarua.

Amesema kwamba zoezi la uandikishaji lilishaanza tangu januari 2 na litakwenda hadi januari 15, na tarehe 16 zoezi rasmi la usambazaji vyandarua litaanza na kuzifikia Kaya zote ambazo zimeandikishwa.

Aidha, akizungumzia hali ya malaria nchini, ameutaja mkoa wa Shinyanga kuwa  unashika nafasi ya 4 kitaifa, kwa kuwa na maambukizi ya ugonjwa wa maralia kwa asilimia kumi na sita   huku Tabora ikishika nafasi ya kwanza asilimia 24, ya Pili Mtwara asilimia 20, na ya tatu ni Kagera asilimia 18.

Nae mratibu wa elimu kwa umma kutoka wizara ya afya, Happines Nania  amesema kwa mwananchi ambaye atapoteza kadi ambayo alipewa wakati akiandikishwa kwa ajili ya kupewa chandarua, anapaswa kwenda kwenye kituo husika ili apewa chandarua chake sababu taarifa zake zitakuwepo,huku akisisitiza pia utunzaji wa vyandarua hivyo na kuvitumia kwa matumizi sahihi yaliyokusudiwa.

Akifungua kikao kazi hicho Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Faustine Mlyutu, ,ameipongeza serikali kwa kampeni hiyo ya mapambano dhidi ya malaria,na kuwasihi waandishi wa habari kupitia  kalamu zao kuelimisha jamii juu ya matumizi sahihi ya vyandarua vyenye dawa.

Amewasisitiza pia waandishi wa habari kuondoa upotoshaji ambao umekuwa ukienezwa juu ya matumizi ya vyandarua hivyo vyenye dawa, na kusababisha baadhi yao kutovitumia, na kueleza kwamba vyandarua hivyo ni salama na havina madhara yoyote.

“Waandishi wa habari tumieni kalamu zenu kuelimisha jamii juu ya matumizi sahihi ya vyandarua vyenye dawa, ili tuijenge Shinyanga isiyo na Malaria,”amesema Mlyutu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *