Rais Mteule wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kusomewa hukumu yake juu ya kesi inayomkabili ya Utoaji hongo, Jaji wa mahakama ya New York Nchini Marekani Juan Merchan anatarajiwa kutoa uamuzi huo juu ya kesi hiyo siku 10 kabla ya kuapishwa kwa Trump Januari 20.
Jaji Merchan amesema Trump, Rais wa kwanza wa zamani kuwahi kuhukumiwa kwa uhalifu, anaweza kujitokeza moja kwa moja Mahakamani au akashiriki kwa njia ya mtandao katika hukumu iliyopangwa kusomwa Januari 10, 2025.
Trump alipatikana na hatia huko New York mnamo kwa makosa 34 ya kughushi rekodi za biashara ili kuficha malipo ya pesa kwa nyota wa filamu za ngono Stormy Daniels kabla ya uchaguzi wa 2016.
Katika uamuzi wenye kurasa 18, Merchan alikataa hoja mbalimbali za mawakili wa Trump wakitaka hukumu yake kutupiliwa mbali ambapo jaji huyo amebainisha kwamba hana nia ya kutoa adhabu ya kifungo jela, badala yake anaegemea katika kuachiliwa bila masharti, hukumu nyepesi ambayo itamfanya Trump aingie Ikulu ya White House kama mhalifu aliyepatikana na hatia.
Kwa upande wa Mawakili wake walikuwa wakitaka kesi hiyo itupiliwe mbali kwa misingi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na uamuzi wa kihistoria wa Mahakama ya Juu mwaka jana kwamba marais wa zamani wa Marekani wana kinga ya kutoshtakiwa kutokana na vitendo mbalimbali vya kiofisi vilivyofanywa wakiwa madarakani.
Hata hivyo Jaji Merchan alikataa hoja hiyo na kubainisha kuwa Trump hataweza kuhukumiwa mara tu atakapoapishwa kama Rais.