Jeshi la zimamoto na uokoaji wilayani Kahama mkoani Shinyanga limewataka wamiliki wa mabwawa ya kuogelea (Swimming Pool) na sehemu za michezo ya watoto kuweka vifaa vya uokozi na huduma ya kwanza katika maeneo hayo ili kuweka tahadhari kwa watu wanaoogelea na kucheza katika maeneo hayo.
Wito huo umetolewa na Mkaguzi Msaidizi, Hafidhi Omari, Mkuu wa kituo jeshi la zima moto wilayani Kahama wakati wakitoa elimu ya kiusalama katika sehemu za kuogelea na sehemu ya michezo ya Watoto.
Omari amesema kuwa watu wengi hawajui umuhimu wa makoti ya kuokolea katika sehemu za kuogelea na kwamba wengi wao hawajui kuogelea hivyo uwepo wa vifaa vya maokozi utasaidia kupunguza ajali na matukio ya watu kupoteza maisha.
“Haya makoti siyo urembo bali yametengenezwa maalumu kwa ajili ya kusaidia mtu asizame pindi anapoogelea, Sasa tumeona maeneo mengi hayana hivi vifaa hivyo wamiliki wa sehemu za kuogelea hakikisheni mnanunua vifaa hivi” Amesema Omary.
Katia hatua nyingine Omari amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa vifaa vya huduma ya kwanza maeneo ya kuchezea Watoto kwa kuwa maeneo hayo yana vitu vingi vikiwemo vifaa vya chuma na kwamba hali hiyo itasaidia kumpa huduma ya haraka mtoto au mtu yeyote ambaye ataumia katika eneo hilo.
“Huduma ya kwanza ni jambo muhimu katika eneo hili,mtu anaweza kuumia lakini kukiwepo sanduku la huduma ya kwanza itakuwa rahisi kumpa huduma kabla hajaenda kupata matibabu makubwa, Kwa hiyo nasisitiza maeneo yote kuwekwe huduma hiyo” Aliongeza Omary.
Kwa upande wake Mustapha Abdul kutoka kitengo cha uokozi na majanga amewataka wananchi kutoa taarifa za haraka pindi linapotokea tatizo katika maeneo yao kwa kupiga simu ya bure namba 114 na kusisitiza matumizi sahihi ya namba hiyo.
“Sisi tupo macho masaa yote ofisi zetu hazifungwi mnapopata tatizo msiache kutoa taarifa kwa kupiga namba 114, namba hizi ni bure kabisa, Ila nasisitiza matumizi sahihi ya namba hii kwani kuna baadhi yenu wanapiga simu na hakuna tukio” Alisema Mustapha.
Nao baadhi ya Wazazi na Watoto waliopata elimu hiyo wamelishukuru jeshi la zimamoto na uokoaji kwa elimu waliyotoa na kwamba imewasaidia kujua umuhimu wa vifaa vya uokozi na kuhaidi kuzingatia pindi wanapotaka kuogelea na kuwapeleka Watoto wao sehemu za michezo hiyo.
“Kwa kweli mimi kama mzazi elimu hii nimeipata na nimefurahi sana,Watoto walikuwa wanaogelea bila kuvaa makoti haya kwa kweli hii imetupa funzo na daima tutazingatia ili kuwafanya Watoto wetu wawe sehemu salama” Alisema Rajabu Mussa mmoja wa wazazi.
Jeshi la zima moto na uokoaji wilayani Kahama limezunguka katika sehemu mbalimbli za kuogelea na michezo ya Watoto ili kutoa elimu ya umuhimu wa kuwa na vifaa vya uokozi, Jinsi ya kutumia vifaa hivyo, Uwepo wa sanduku la huduma ya kwanza Pamoja na elimu ya uzingatiaji wa utaratibu wa kuingia kwenye bwawa la kuogelea.