Kipa wa Simba Moussa Camara amezidi kujiweka katika nafasi nzuri baada ya kucheza michezo 12 bila kuruhusu bao katika michezo 15 ya Ligi Kuu ya NBC aliyocheza.
Golikipa huyo aliyesajiliwa na Simba msimu huu ameonekana kama ‘lulu’ baada ya kuruhusu mabao Matano tu katika michezo yote aliyocheza huku timu yake ikiwa imefunga mabao 31 na kufanikiwa kuwa kileleni mwa msimamo wa ‘Cleansheet’ ndani ya Ligi Kuu ya NBC.
Camara alifungwa na Yanga Oktoba 19 katika dabi ya kariakoo goli walilojifunga Simba kupitia mchezaji wao Kelvin Kijili hivyo mchezo kumalizika kwa Yanga kushinda mchezo huo muhimu.
Katika mchezo wa Simba dhidi ya Coastal Union uliochezwa uwanja wa KMC, Camara aliruhusu mabao mawili kipindi cha pili cha mchezo huo na pia mchezo wa Kagera Sugar dhidi ya Simba uliochezwa uwanja wa Kaitaba Simba walishinda mabao matano huku wakiruhusu mabao mawili.
Patrick Munthali wa Mashujaa anashika nafasi ya pili kwenye msimamo huo baada ya kufanikiwa kukusanya nane katika michezo 16 ambayo timu yake imecheza.
Nafasi ya tatu inashikiliwa na Djigui Diarra akiwa amekusanya saba sawa na Metacha Mnata wa Singida Big Stars.
Kipa wa Azam Mohamed Mustapha naye yupo katika orodha hii baada ya kufanikiwa kukusanya sita huku timu yake ikiwa na alama 36 kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wakiwa wameruhusu mabao nane na wakifunga mabao 25.