Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar (ZDCEA) kwa kushirikiana na vyombo vyengine vya Ulinzi na Usalama imefanya operesheni maalum za kimkakati na kufanikiwa kukamata jumla ya 798.893 kg za Dawa za kulevya aina Bangi, Cocaine, Heroin, Methampetamine na shisha zilizochanganywa na dawa za kulevya aina mbalimbali.
Katika Operesheni hiyo jumla ya gari 6, boti 1 na watuhumiwa 9 kati yao 8 ni raia wa Tanzania na 1 ni raia wa kigeni, ambapo wote wamekamatwa kwa tuhuma za kuhusika na dawa hizo na baadhi yao tayari wamefkishwa Mahakamani na wengine watafikishwa mara baada ya taratibu za kisheria kukamilika.
“Kiwango kilichokamatwa ni kikubwa ambacho hakijawahi kukamatwa katika historia ya Zanzibar tangu Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964. Dawa hizo zingefanikiwa kuchepushwa na kuingia mtaani zinaweza kutengeneza kete milioni 27 wakati idadi ya watu wote Unguja na Pemba ni milioni 1.8 kwa mujibu wa Sensa ya watu na maakazi ya mwaka 2022, kete hizo ukigawa kwa idadi ya watu unapata wastani wa kete 14 kwa kila mtu aliyopo Zanzibar Tunaeleza haya ili wananchi wenzangu waweze kupata picha halisi ya wingi wa dawa za kulevya aina ya Methampetamine zilizokamatwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya katika kipindi cha 2′ – Kanal Burhan Nassor Kamishna wa Mamlaka ya Madawa Zanzibar.