Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar ZDCE imefanya operesheni Novemba 05 Mwaka huu katika Viwanja vya Ndege vya kimataifa Abeid Amaan Karume na kufanikiwa kukamata Shisha boksi 15 sawa na Pisi 300 zenye Uzito wa 263 Kg zilizoingizwa kutoka China ambapo mwaka jana Zanzibar ilipiga marufuku uingizaji na utumiaji wa shisha Visiwani Zanzibar.
Kamishna wa Mamlaka hiyo Kanal Burhan Nassor akizungumza na Waandishi wa habari amesema mara baada ya kukamatwa kwa shisha hizo mamlaka ilimbaini muingizaji ni Alperen karakurum Raia wa Uturuki Mkazi wa Dar es Salaam ambapo shisha hizo zilifanyiwa uchunguzi wa kitaalamu katika maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kubainika kuwa ndani yake kuna Kemikali mbalimbali ikiwemo kemikali ya “Bufotenin’
ambazo zinapumbaza akili ya mtumiaji (hallucination) na kusababisha athari mbalimbali za kiafya ikiwemo magonjwa ya moyo, uraibu, kiwewe na kuchanganyikiwa hali inayoweza kupelekea mtu kujidhuru au kudhuru watu wengine.
Shisha hizo zimewekwa ladha mbalimbali kama strawbery mango, Mango Passion Fruit, Red Energy, Purple Rain, Grape, Cool Mint, blueberry ice na Water Melon Bubble Gum ili kuwavutia watumiaji. Aidha, shisha zilizokamatwa zinafanana sana na zile zinazouzwa katika maduka ya supermarket mbalimbali ambazo zinatumiwa zaidi na vijana hasa wanawake kutokana na kuwekwa ladha zenye kuvutia watumiaji.
Aidha, kupitia operesheni hiyo, Mamlaka imefanikiwa kuzuia kuingizwa nchini kwa shisha nyengine zaidi ya boksi 295 ambazo ndani yake kuna pisi 59,000 zenye uzito wa 500 kg sawa na nusu tani zilizokuwa tayari zimeshalipiwa na mfanyabiashara huyo kwa ajili ya kuingizwa Tanzania kutoka China.