RC MTANDA AKASIRIKA HOSPITALI YA UKEREWE KUTOKAMILIKA, ATOA MAELEKEZO HAYA…

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amemuagiza Katibu Tawala kumpeleka Mkaguzi wa ndani wa Mkoa kukagua mwenendo wa utekelezaji wa ujenzi wa Jengo la wazazi katika Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe kabla hajachukua hatua kwa wazembe watakaobainika.

Mtanda ametoa agizo hilo mapema leo ijumaa tarehe 27 Desemba, 2024 wakati alipotembelea hospitalini hapo kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la wazazi na kubaini kuna ucheleweshaji wa miezi 6 kinyume na mkataba na akaagiza ndani ya siku 20 likamilike.

“Serikali imeleta milioni 900 kwenye hospitali hii kwa ajili ya kujenga wodi muhimu ya wazazi ili kuboresha huduma bora za afya kwa wananchi na kuboresha hali ya utoaji huduma hivyo wasimamizi hampaswi kukwamisha juhudi hizi”. Mhe. Mtanda.

Ameongeza kuwa inashangaza kuona fedha zimeshafika tangu mwezi Machi mwaka huu na walipaswa kukamilisha ujenzi mwezi Juni lakini ni milioni 700 pekee zimelipwa kwa mafundi ikiwa ni asilimia 85 ya fedha zote na kusababisha kuchelewesha ujenzi huo.

Aidha, ameelekeza mzabuni wa milango kwenye hospitali hiyo ahakikishe anakabidhi mara moja ili iweze kuwekwa na kukamilisha ujenzi na kuhusu majengo yaliyotelekezwa yaliyoandaliwa kufanya upanuzi ameahidi kuwasiliana na wizara ili kuhakikisha fedha zinaletwa kukamilisha ujenzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *