‘KUWENI MAKINI NA WATU WANAOTAKA KUWAGOMBANISHA NA SERIKALI’ – RC KENANI…

NA SAADA ALMASI -SIMIYU

Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mh. Kenani Kihongosi amewataka Wafanyabiashara mkoani Simiyu kuwa makini na watu wanaotaka kuwagombanisha na serikali kwa kuanzisha vurugu zinazokuja kuwagharimu katika mitaji ya biashara zao.

RC Kenani ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Wafanyabiashara katika kikao cha Baraza la biashara mkoa, muda mfupi baada ya kugawa vitambulisho kwa wafanyabiashara hao akisema kwamba kati yao wataibuka watu na kuwahamasisha wafanye migomo na maandamano lakini kiuhalisia hasara za hizo vurugu ni kubwa

“Sitarajii kuona maandamano wala vurugu zozote na niwaambie wapo watu watakao hamasisha vurugu na mkiitikia wanakuja kuharibu mali zenu maduka yatavunjwa bidhaa zitaibiwa na mwisho inakuwa hasara kwenu” amesema kenani.

Sambamba na hilo, Kenani amewataka wajitokeze kwa wingi katika kulipia vitambulisho vyao ili waweze kupata fursa za mikopo katika taasisi mbalimbali za fedha huku akimuagiza katibu tawala na viongozi wengine kuendelea kutoa hamasa kwa wengine ambao hawajapata vitambulisho waweze kulipia

“Mjasiriamali anakwenda kupata faida kwa kupata huduma za mikopo kutoka taasisi mbalimbali za kifedha na nitoe rai kwa katibu tawala kuendelea kutoa elimu ili wajasiria mali wengi zaidi wajitokeze kulipia vitambulisho hivi” Kenani.

Kwa upande wake katibu tawala wa mkoa, Prisca Kayombo amesema kuwa ofisi ya mkoa iko tayari kupokea malalamiko yoyote ya Wafanyabiashara na kuyatafututia ufumbuzi hivyo wawe na desturi ya kujitokeza katika mabaraza ya wilaya na kueleza changamoto zao ili zifikishwe katika mkoa

“katika ngazi ya wilaya haya mabaraza yanaumuhimu sana jitokezeni kushiriki na mpeleke malalamiko yenu ili sisi kama mkoa tukiletewa tuyatafutie ufumbuzi ili muweze kufanya biashara katika kazingira mazuri na yenye utulivu” amesema prisca.

Mwenyekiti wa wajasiriamali mkoa wa Simiyu, Thomas Mashalo amesema kuwa hatoruhusu mtu yeyote kufanya biashara bila kuwa na kitambulisho chenye picha yake ili aweze kudhibiti vitendo vya wizi na vibaka ambao wamekuwa wakimsumbua mara kwa mara 

“Juzi tu nimepokea kesi ya wizi na sasa hivi yupo polisi kwa hiyo sinto ruhusu mfanyabiashara yeyote kufanya biashara bila kutambulika kwa kuwa wengi wao huwa ni wezi na vibaka” amesema Thomas

Lucia Baraza ni mjasiriamali ambaye tayari anamiliki kitambulsho chake amesema kuwa mwanzoni alikuwa wanakamatwa kiholea na kutozwa ushuru ambao haukuwa na kiwango maalum hivyo hakujua kama pesa hizo zinakwenda sehemu sahihi ama la lakini kwa sasa anauhakika anachangia maendeleo ya taifa lake.

“Muda wowote unaweza kukamatwa unadaiwa ushuru na haijalishi ni kiasi gani na yule mtu hakupi risiti sasa sina uhakika hiyo pesa inaishia wapi lakini kwa sasa hata nikitoa najua kabisa pesa nimechangia maendeleo ya nchi”amesema Lucia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *