Jeshi la Polisi limetoa ufafanuzi wa taarifa iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii inayomhusu Mchezaji Bernard Morrison ikituhumu Kituo cha Polisi Mbweni kilichopo Jijini Dar es salaam.
Ufatanuzi uliotolea na Jeshi la Polisi unasema, Bernard Morrison Machi, 2024 alifungua kesi ya Wizi wa Kuaminiwa katika Kituo cha Polisi Mbweni kuwa, akiwa Ghana alimtumia Abdul Rakeeb Mgaya kiasi cha shilingi milioni moja na laki tano (1,500,000) ili amkabidhi mdogo wake aliyemtaja kwa jina la Boat anayeishi hapa Nchini kumtafutia timu itakayo msajili lakini hakufanya hivyo.
Baada ya malalamiko hayo aliyetuhumiwa alitafutwa na alipohojiwa alieleza ni kweli alitumiwa hizo fedha ili zisaidie kwenye gharama za kumsajili huyo mdogo wake lakini ilishindikana kwasababu hakuwa na kiwango cha kusajiliwa na timu aliyokuwa anahitaji.
Hata hivyo, alimtaka Bemard Morrison ampe muda atamrejeshea fedha zake. Pia alielezwa kulingana na ushahidi hakuna kesi ya jinai. Hivyo walielewana na kwa vile wote ni raia wa Ghana walikubaliana kulipana.
Juni 3,2024 iliripotiwa kesi ya kuharibu mali ambapo Bernard Morrison akiwa na mdogo wake na mtu mwingine walifika nyumbani kwa Abdul Rakeeb na kuvunja geti kisha kuchukuwa kwa nguvu gari aina ya IST namba T239 DFM.
Bernard Morrison aliendelea kutafutwa bila mafanikio lakini Abdul Rakeeb alifanikiwa kuliona gari hilo likiwa limeegeshwa sehemu na kulichukuwa na kulipeleka Kituo cha Polisi Mbweni.
Jeshi la Polisi limemwambia Bernard Morrison anachotakiwa kufanya ni kuacha kujificha, kusema ukweli na kufika kituo cha Polisi kuonana na Uongozi ili sheria ichukue mkondo wake.