RC KIHONGOSI ATOA SIKU 7 KIPINDUPINDU KIISHE SIMIYU.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Kenan Kihongosi ametoa siku 7 kwa wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri Mkoani humo kumaliza ugonjwa wa Kipindupindu.

Aidha amewaagiza wakuu wa Wilaya na wakurugenzi Mkoani Simiyu kusimamia Sheria ndogo za Halmashauri kwa  kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kukiuka kanuni za Afya na usafi wa mazingira  ili kutokomeza kipindupindu Mkoani humo.

Mhe.Kihongosi ametoa rai hiyo katika kikao kilichokutanisha Viongozi kutoka Taasisi  mbalimbali  Mkoani Simiyu katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa ulioko katika Mji wa Kiserikali Nyaumata Wilayani Bariadi kilichoketi kwa lengo la kujadili mikakati ya kupambana na ugonjwa wa kipindupindu.

“Hakuna aliye juu ya Sheria,tusioneane aibu,tuwajibike kutokomeza kipindupindu”Alisema Mkuu wa Mkoa Kihongosi.

Mhe.Kihongosi amesema kuwa baadhi ya  Wanasiasa Mkoani humo  wamekuwa wakikwamisha mapambano ya ugonjwa wa kipindupindu Mkoani Simiyu jambo linalochangia kuendelea kushamiri ugonjwa huo mkoani Simiyu.

Kutokana na changamoto hiyo,amesema  hatofumbia macho kiongozi yeyote atakaekwamisha jitihada za Serikali katika mapambano ya ugonjwa hatari wa  kipindupindu unaohatarisha maisha ya Wananchi Mkoani Simiyu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *