TUNDU LISSU ACHUKUA FOMU YA KUGOMBEA UENYEKITI CHADEMA TAIFA.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tanzania Bara Tundu Antipas Lissu leo Disemba 17 amefika Makao Makuu ya Chama hicho Mikocheni Jijini Dar es salaam kwa ajili ya kuchukua fomu na tayari amechukua fomu ya kugombea Uenyekiti wa Chama hicho Taifa nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na Freeman Mbowe.

Mara baada ya kukabidhiwa fomu hizo Tundu Lissu alielezea watu waliomuunga mkono kwenye suala lake la kuchukua fomu ambapo amesema ‘Hizi fomu za kugombea Uenyekiti wa CHADEMA Taifa ada yake ni Tsh. milioni 1.5, ningeilipia mwenyewe lakini kuna Wanachama wema wanaofikiri kama Mimi, wanaofikiri kwamba Uchaguzi huu uwe mwanzo mpya kwa Chama chetu ambao wamechanga fedha ya kulipia gharama ya kuchukua fomu lakini hata hivyo hiyo fedha waliyochanga Wanachama haitatumika kulipia hizo fomu na fedha yangu mwenyewe vilevile haitotumika kulipia hizi fomu” – Tundu Lissu.

Tundu Lissu ameongeza kwa kusema ‘Hiyo Tsh. milioni 1.5 inayotakiwa kulipia hizi fomu imetolewa na Mwanachama wetu mmoja anayeitwa Edgar Edson Mwakabela kwa jina maarufu Sativa ambaye alikamatwa na Watu wa Usalama wa Nchi hii akateswa vibaya sana, akapigwa risasi na kutupwa porini Katavi, Mungu sio Athumani Sativa yupo hai leo yupo uhamishoni ilibidi akimbie Tanzania ili wasimmalizie na amenipigia akasema naomba nikulipie fomu kwasababu naamini ukiwa Mwenyekiti wa hiki Chama utafanya ile kazi inayohitajika ya kupigania haki za Watanzania ” — Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti CHADEMA Tanzania Bara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *