Categories

Do you have a Story?

Call us on 0677 644 444 to submit your news story or incident report!

Bil.22 Kutekeleza Ujenzi Masoko Mawili Ya Samaki Mwanza.

Na Melkizedeck Anthony


Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 22 kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa masoko mawili ya kisasa ya samaki katika mkoa wa Mwanza zoezi ambalo linatarajia kuanza Novemba 1, Mwaka huu.


Ujenzi huo utahusisha Soko la Samaki Kirumba katika Manispaa ya Ilemela litakalogharimu zaidi ya Sh.bilioni 14.7 pamoja na Soko la Samaki Mkuyuni katika Jiji la Mwanza linalogharimu zaidi Sh.bilioni 7.36 na utekelezwaji wake utafanyika kupitia Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Miji ya Tanzania (TACTIC) kupitia mkopo wa Benki ya Dunia(WB).


Akizungumza wakati wa utiaji saini wa mikataba hiyo miwili, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa amesema ujenzi huo unalenga kuongeza kasi ya maendeleo hapa nchini hususani kwa wafanyabishara wa Samaki pamoja na wananchi wote kwa ujumla.


Katika hatua nyingine Mchengerwa amewaagiza wakandarasi wote wanaotekeleza miradi yote ya barabara chini ya Mradi wa TACTIC kuhakikisha ujenzi wake unakamilika kwa wakati na kuwa hakutakuwa na ongezeko la muda tofauti na ule uliopangwa kimkataba.


“Wakuu wa mikoa simamieni hawa wakandarasi wahakikishe wanatekeleza miradi kwa wakati kwani hatutomuongezea muda Mkandarasi yeyote,” alisema Mchengerwa
Aidha Mchengerwa amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TARURA kuhakikisha anaanza utekelezaji wa ujenzi wa barabara yenye urefu wa km 10 iliyopo jijini Mwanza kwa kiwango cha lami na kueleza kuwa serikali haiwezi kuvumilia kuwa na barabara katikati ya majiji ambazo hazijajengwa kwa kiwango cha lami na kwamba wakurugenzi wa halmashauri zote wanatakiwa kusimamia ipasavyo miradi yote inayotekelezwa chini ya wizara hiyo.


Awali akitoa taarifa ya miradi hiyo pamoja na mingine inayotekelezwa mkoani Mwanza na nchini kwa ujumla kupitia TACTIC inayosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mtendaji Mkuu wa Wakala huo, Mhandisi Victor Seff amesema miradi yote inagharimu zaidi ya dola za marekani milioni 410.


Mhandisi Victor amesema lengo la mradi huo wa TACTIC ni kuboresha miundombinu ya Miji 45 ya Tanzania pamoja na kujengea uwezo Halmashauri ili ziweze kuimarisha usimamizi wa uendelezaji wa miji pamoja na ukusanyaji wa mapato.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *