Categories

Do you have a Story?

Call us on 0677 644 444 to submit your news story or incident report!

Wanawake Wahimizwa Kuchukua Mikopo Inayotolewa Na Serikali Kujikwamua Kiuchumi

Na Gideon Gregory

Kaimu Afisa Ustawi wa Jamii Jijini Dodoma Dkt. Faudhia Mohamed ametoa rai kwa wanawake kwenda katika Halmashauri kuchukua mikopo ya akina mama inayotolewa na Serikali ili kuweza kujikwamua kiuchumi pamoja na kuchangamkia fursa zilizopo katika maeneo yao.


Dkt. Faudhia ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akiongoza Maadhimisho ya siku ya Mwanamke anayeishi Kijijini yaliyofanyika katika Kata ya Mpunguzi yenye kauli mbiu ya “Wezesha mwanamke aishiye Kijijini kutumia nishati safi na salama, shiriki uchaguzi wa serikali za mitaa.


“Twendeni Halmashauri tuchukue mikopo, hii mikopo ipo kweli na wenzetu wanafaidika nayo kwahiyo na nyie wanawake wa vijijini mkienda kukopa mtafaidika nayo mkienda kukopa nendeni kwa vikundi vyenu mkishachukua mtaongezea kwenye mitaji yenu kwasababu mwenye nacho anaongezewa,” amesema Dkt. Faudhia.


Aidha amewaomba wanawake hao kuhakikisha wanasimamia vyema suala la elimu kwa watoto wa kike ili waweze kujitetea juu ya changamoto zinazowakabili katika jamii pamoja na kupatiwa haki zao za msingi.


“Baadhi yenu watoto wa kike hamuwapeleki shule mnawaacha wanakaa nyumbani wanafanya kazi za ndani hawapati elimu na hii ni shida kubwa sana wakikosa elimu wanashindwa kujisimamia kwa hiyo sisi kama wazazi tunapaswa kuhakikisha watoto wetu wa kike wanapata elimu, “amesema Dkt. Faudhia.


Ameongeza kuwa endapo mzazi ataona watoto wakike hawataki kwenda shuleni ni vyema akaomba msaada kwa walimu kwani wapo kwaajili ya kuwasaidia hivyo wasisite kuwafata ili suala hilo liweze kupatiwa ufumbuzi wa kina zaidi.


Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Shirika la Kimataifa la Milki ya Ardhi na Haki za Ardhi (LANDESA) Hadija Mrisho amesema kufuatia elimu wanayoitoa wamefanikiwa kuwezesha wanawake wengi waliopo vijijini kumiliki ardhi kwa kiasi kikubwa kutokana na utambuzi walionao kwasasa.

“Suala la kumiliki ardhi linaanza na utambuzi kwasababu ukishatambua kwamba nina haki ya kumiliki na kupata ardhi pamoja na kufanya maamuzi basi utaweza kuamka ili uweze kupata haki yako ya msingi ya kuanza miliki ardhi,”amesema Bi Hadija.


Wakili kutoka chama cha wanasheria wanawake Tanzania Isabella Nchimbi amewaomba watanzania kuheshimu haki za binadamu ikiwa ni pamoja na haki ya kumiliki ardhi ambayo kisheria kila mtu anayo haki hiyo licha ya kuwepo kwa mila kandamizi ambazo zimekuwa zikimnyima mwanamke kumiliki ardhi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *