Categories

Do you have a Story?

Call us on 0677 644 444 to submit your news story or incident report!

Rais Samia Asisitiza Utunzaji Wa Mazingira Katika Kukabiliana Na Athari Za Tabianchi

Na Melkizedeck Antony

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan ameitaka jamii kuzingatia suala la utunzaji wa mazingira ili kukabiliana na athari za tabianchi zinazoikumba Tanzania pamoja na dunia kwa ujumla.


Dk Samia ameyasema hayo wakati wa kilele cha mbio za mwenge zilizofanyika jijini Mwanza ambapo amesema suala la uchafuzi wa mazingira kwa kiasi kikubwa linasababishwa na shughuli za kibinadamu kama vile uharibifu wa vyanzo vya maji, uchomaji wa misitu, uchimbaji wa madini ,ukataji holela wa miti pamoja na vitu vingine kama hivyo.


“uhifadhi wa mazingira ni moja ya ujumbe wa mwenge huu wa uhuru ambao pia ni moja ya changamoto kubwa inayoikabili dunia kwa sasa kwa upande wetu Tanzania uchafuzi wa mazingira unasababishwa na shughuli za kibinadamu kama vile uvamizi wa maeneo tengefu kwa ajili ya malisho na kilimo, uharibifu wa vyanzo vya maji, kuishi na kulima milimani, shughuli za uchimbaji wa madini, ukataji holela wa miti, uchomaji wa mapori na misitu mambo yote haya yana mchango katika uharibifu wa mazingita hapa nchini”


Katika hatua nyingine Dk. Samia amesema kutokana na uharibifu wa mazingira hali hiyo inaweza kupelekea upungufu wa mvua , mvua zisizotabirika pamoja na ukame hivyo amezitaka mamlaka zinazosimamia mazingira kuhakikisha sheria za usimamizi wa mazingira zinatekelezwa kikamilifu ili kuwa na mazingira bora.


Kuhusiana na suala la mbio za mwenge Rais Samia amesema amesikiliza kwa umakini taarifa iliyotolewa na wakimbiza mwenge mwaka huu na ameona maeneo mbalimbali yakilalamikiwa kubwa zaidi ikiwa ni katika suala la barabara, na kama serikali wamepokea maoni, ushauri pamoja na mapendekezo yote yaliyotolewa na wakimbiza mwenge na wanakwenda kuyafanyia kazi.


Aidha amesema katika suala la uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa mwenge wa uhuru umetoa ujumbe ukiwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo kwani kupitia uchaguzi huo ndio sehemu pekee ambayo mwananchi anayo fursa ya kumpata kiongozi ambaye atawatumikia katika mifumo yote ya utawala.


Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete amesema Mbio za mwenge zimefanikiwa kutembelea miradi ya kimaendeleo 1,595 yenye thamani ya shilingi trilioni 11 na miradi hiyo imeweza kuzinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi huku miradi 16 yenye thamani ya shilingi bilioni 8.6 ikikataliwa na mwenge huo na tayari imekabidhiwa kwa mamlaka ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU kwa ajili ya uchunguzi zaidi.


“Mheshimiwa Rais miradi ya maendeleo elfu moja mitano tisini na tano yenye thamani ya shilingi trilioni kumi na moja imeweza kuzinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi ikilinganisha na miradi elfu moja mia nne na ishirini na nne yenye thamani ya shilingi trilioni tano nukta tatu iliyokaguliwa mwaka 2023”


“ Mheshimiwa raisi naomba kutoa taarifa miradi kumi na sita yenye thamani ya shilingi bilioni nane nukta sita iliyokataliwa na mwenge wa uhuru na tayari imekabidhiwa kwa mamlaka ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU kwa ajili ya uchunguzi”


Katika hatua nyingine Ridhiwani amesema katika kupambana na maambukizi ya virusi vya ukimwi wananchi elfu sitini na sita na sitini na mbili wamepima virusi vya ukimwi kwa hiari ambapo watu mianne tisini na nane sawa na asilimia sifuri nukta nane ya waliojitokeza wana maambukizi ya ukimwi.


Aidha amesema katika mapambano ya Malaria jumla ya watu 25,879 walijitokeza kupima maambukizi ya ugonjwa huo ambapo kati ta wananchi 1121 sawa na asilimia 4.3 walibainika kuwa na vimelea vya ugonjwa wa malaria na walipatiwa huduma stahiki.


Akisoma taarifa ya mbio za Mwenge kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Godfrey Mzava amesema Mbio za mwenge zimebaini changamoto kubwa ya ukataji wa kodi za fedha zinazoletwa na serikali ajili ya miradi ya maendeleo kwani taasisi husika hazitimizi wajibu wake katika kuhakikisha kodi hizo zinakatwa na kurudishwa katika mamlaka ya mapato Tanzania TRA.


Katika hatua nyingine Mzava amesema ipo changamto ya zabuni za manunuzi ya serikali kuwa zinatolewa nje ya mfumo wa kidigitali wa manunuzi ya umma (NEST) jambo ambalo ni kinyume na sheria ya manunuzi kwa Umma ya mwaka 2023 na ni kiashiria cha ubadhilifu wa mali za umma.


Pia amesema mwenge huo wa uhuru umezunguka katika mikoa yote 36 kama ilivyotakiwa ambapo katika maeneo ambayo mwenge huo ulipita wananchi wa maeneo hayo walitoa maombi mbalimbali kwa serikali ambapo kwa mkoa wa shinyanga wameomba serikali kuwajengea barabara ya Kolandoto – Muhenza pamoja na barabara ya Ushetu- kahama kwa kiwango cha lami ili kurahisisha shughuli za usafiri pamoja na usafirishaji.


Mara baada ya kufanyika kwa kilele cha mbio za mwenge jijini Mwanza, Mwenge huo umekabidhiwa kwa Jeshi la wananchi JWTZ kwa ajili ya kuanza safari ya kuelekea katika mkoa wa Kilimanjaro ambapo unatarajia kuwasili Octoba 15, 2024 kisha kupandishwa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *