Categories

Do you have a Story?

Call us on 0677 644 444 to submit your news story or incident report!

Taifa Limefanya Ibada Kumuombea Hayati Mwl.Julius Kambarage Nyerere

Na Melkizedeck Antony

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza Mhashamu Renatus Nkwande amewataka wananchi wote hapa nchini kuheshimu hatua za maendeleo zilizofikiwa na Taifa kwani kutimiza Miaka 60 ya mbio za mwenge ni jambo la kujivunia.


Askofu Nkwande amesema hayo mapema leo Oktoba 14, 2024 wakati wa ibada ya kumuombea Hayati Mwl.Julius Kambarage Nyerere iliyofanyika katika Parokia katoliki ya Mt. Fransisco wa Exavery Nyakahoja jijini Mwanza iliyoanza saa 12:00 asubuhi.


Ibada hiyo imehudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Dk.Philp Mpango, Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pamoja na viongozi wengine wengi wa serikali na vyama vya kisiasa.


Akizungumza katika ibada hiyo Askofu Nkwande amesema
“Miaka 60 iliyopita maisha hayakuwa kama ya leo hata miaka 50 ninayoifahamu mimi tofauti ipo kuna wakati mimi niliishi Musoma miaka fulani baada ya vita maisha tuliyokuwa nayo yalikuwa ni maisha magumu ya ovyo na wakati mwingine tulivuka ng’ambo kwenda Kenya ili tukanunue mche wa sabuni, dawa ya meno hapa kwetu hakukuwa na kitu,”


Aidha askofu Nkwande amesema kwa miaka yote hiyo nchi imefika ilipo kwa juhudi za watanzania wenyewe pamoja na viongozi walioongoza hivyo hakuna budi kuwapenda na kuthamini mchango wao.


Kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, Askofu Nkwande aliwataka watanzania kushiriki kwa hekima na busara na siyo kupambania madaraka.
“Huwa najiuliza hivi na mimi nisingekuwa padre ningegombania jinsi hii?, unakuta mtu anakakamia na mishipa inamtoka anataka awe mbunge anadiliki hata ampige mwenzake, hatujafika huku kama walipofikia wengine huko,”


Akizungumza kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Dk.Philp Mpango amesema dhumuni la kufanya ibada hiyo ni kumuombea Baba wa Taifa Mwl.J.K.Nyerere ili hata Rais pamoja na wasaidizi wake wajaliwe hekima ya kuwatumikia watanzania.


“Baba wa Taifa aliongoza kwa ustadi katika kuwaunganisha watanzania na kuzifanya kabila zaidi ya 120 na kuwa kitu kimoja sambamba na kutuunganisha kwa lugha moja ya Kiswahili,”amesema Dk.Mpango.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *