Wanawake Walia Kutonufaishwa na Fedha za Tumbaku

Na William Bundala,Kahama

Wanawake wa kata ya Ulowa halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamelalamikia kitendo cha baadhi ya wanaume wao kuwanyima fedha za malipo ya Tumbaku baada ya kuuza na badala yake kutumia fedha hizo kwenye starehe kwa kuoa wanawake wengine,kuwa na nyumba ndogo na kuzamia katika matumizi ya pombe.

Wakizungumza na Jambo Fm,wanawake hao wamesema wamekuwa wakitumia muda mrefu katika kilimo cha Tumbaku lakini hawanufaiki na matunda ya kilimo kutokana na baadhi ya wanaume kuwapiga na kuwafukuza pindi wanapohoji kuhusianana na  fedha za malipo ya Tumbaku baada ya mavuno kuuzwa.

“Mwanaume anapoenda kupokea pesa hakumbuki tena mke wake nyumbani,wanaishia Senta anatumia hela,anamaliza na makahaba na mwanamke akizungumza juu ya hilo anapigwa,anafukuzwa,anaambiwa nenda kwenu”,amesema mmoja kati ya wanawake hao ambaye hakutaka jina lake litajwe

Sambamba na hayo wanawake hao wameiomba serikali kuanzia ngazi ya kata kuwaondoa wanawake waliokwenda kufanya biashara ya ukahaba kwenye kata hiyo wakati huu wa msimu wa mavuno wakielezea kuwa wanawake hao ndiyo chanzo cha wanaume kutelekeza familia na pia kuchangia kuchangia mmomonyoko wa maadili kwa watoto wao.

Kwa upande wake diwani wa Kata ya Ulowa Gabriela Kimaro amekiri kuwepo kwa tabia ya wanaume kuwanyanyasa wake zao kwa kuwanyima fedha za tumbaku baada ya kuuza na kutoa wito kwa wanaume kutambua mchango wa wanawake wakati wa utafutaji wa kiuchumi na kwamba ndoa nyingi zinavunjika wakati wa msimu wa malipo ya tumbaku.

Kata ya Ulowa ina vijiji sita na vyote vinategemea tumbaku kama zao kuu la biashara huku wananchi wa kata hiyo wakitegemea zao hilo kwa 80% kuendesha maisha yao kila siku.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *