Na Gideon Gregory,Dodoma
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro amesema Serikali inayo mikakati mbalimbali ya kuwawezesha wadau wake kuwekeza katika kuzalisha vipaji vya michezo hususan mpira wa miguu ikiwemo kuandaa miongozo na kanuni mahususi zinazowalinda wadau wanaoanzisha shule maalumu za kukuza na kuendeleza vipaji vya michezo (Sports Academies) ili kuhakikisha wananufaishwa na uwekezaji wanaoufanya.
Dkt. Ndumbaro ameyasema hayo leo Juni 7,2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Norah Waziri Mzeru aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wadau wa michezo kuwekeza katika kuzalisha vipaji vya michezo mbalimbali hasa mpira wa miguu.
Aidha, ameongeza kuwa pamoja na hatua kadhaa nyingine, Serikali inawaunganisha wadau hao na Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania kupitia programu kadhaa za kuibua na kuendeleza vipaji zikiwemo UMITASHUMTA, UMISETA na UMISAVUTA.
“Aidha, Serikali imeanzisha mafunzo ya elimu ya michezo ngazi za Astashahada na Stashahada katika vyuo sita (6) nchini vikiwemo: Vyuo vya Ualimu Butimba, Korogwe, Mpwapwa, Monduli na Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya”,amesema.
Amesema Serikali inaendelea kuimarisha utoaji wa mafunzo ya Shahada ya kwanza katika elimu ya michezo kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa lengo la kuongeza idadi ya wataalamu wa kufundisha michezo ili kupunguza gharama za uwekezaji.