Ripoti ya shirika la Umoja wa mataifa linalohudumia watoto (UNICEF) iliyotolewa Alhamisi Juni 6,2024 inaeleza kwamba,mtoto mmoja kati ya watoto wanne walio na umri wa chini ya miaka mitano wanakabiliwa na umaskini mkubwa wa chakula, na kuwaweka katika hatari ya kukabiliwa na utapiamlo unaotishia maisha yao.
Aidha asilimia 27 ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, sawa na watoto milioni 181 wanapata milo isiyozidi miwili kati ya milo minane inayotambuliwa na UNICEF, kiwango ambacho shirika hilo linakiorodhesha kama umaskini mkubwa wa chakula. Kama watoto hawapati lishe muhimu, kuna hatari wanakuwa na uzito dhaifu wa mwili, aina mbaya sana ya utapiamlo.
Zaidi ya theluthi mbili ya watoto milioni hao 181 wanaoishi na umaskini mkali wa chakula wanaishi Asia Kusini na kusini mwa Jangwa la Sahara, huku nchi 20 zikiwa na asilimia 65 ya watoto wanaoishi na umaskini mkali wa chakula.
Wakati huo huo kwa mujibu wa Ripoti hiyo Umaskini wa chakula huko Gaza umeongezeka sana tangu vita vya Israel dhidi ya Hamas vilipoanza.