Serikali kuja na Tiba Kamili Tatizo la Ajali Barabarani

Na Gideon Gregory,Dodoma

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Jumanne Sagini amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti itakayosaidia kukomesha ajali za barabarani ambayo mingoni mwake ni pamoja na kuifanyia marekebisho Sheria ya Usalama Barabarani ambapo Muswada wa Sheria tayari umewasilishwa Bungeni na kusomwa kwa mara ya kwanza.

Naibu Waziri Sagini ameyasema hayo leo Juni 5,2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani Mh. Hamad Masauni la Mbunge wa Viti maalumu Mhe. Felista Njau aliyetaka kujua Serikali ina mkakati gani madhubuti wa kukomesha kabisa ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikigharimu maisha ya watu wengi.

“Mikakati mingine ni kuboresha miundombinu ya barabara na kuweka alama za matumizi ya barabara, kuandaa utaratibu wa kufunga mifumo ya TEHAMA barabarani ili kufuatilia na kudhibiti ajali, kuandaa utaratibu wa ukaguzi wa lazima wa vyombo vya moto ili kudhibiti ubora wa vyombo hivyo viwapo barabarani”,amesema.

Pia ameongeza kuwa wataendelea kutoa elimu ya Usalama Barabarani kupitia vituo vya Luninga na Redio, Elimu kwenye shule za Msingi, Sekondari na Vyuo, vituo vya mabasi, vituo vya bodaboda na bajaji, vituo vya ukaguzi wa magari, shule za udereva na kutoa mafunzo kwa madereva wa Serikali, Taasisi za Umma na watu binafsi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *