Tume ya uchaguzi ya Afrika Kusini imesema kuwa imekata rufaa katika mahakama ya juu zaidi nchini humo ikiiomba kutoa uamuzi kuhusu iwapo rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma, anaweza kuwa mgombea katika uchaguzi mkuu wa mwezi mei au la.
Rufaa hiyo ni hatua ya karibuni zaidi katika mzozo wa kisheria unaohusu ustahiki wa mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 81 kugombea katika uchaguzi ujao, baada ya mahakama ya uchaguzi kuamua wiki hii kuwa zuma anaweza kuwania nafasi hiyo, na kubatilisha uamuzi wa awali uliokuwa umemzuia kugombea.
Zuma anatarajia kugombea urais kwa tiketi ya chama cha Umkhonto Wesizwe Party (mk), ambacho alijiunga nacho mwaka jana baada ya kukitupia madongo chama tawala cha african national congress (ANC) ambacho aliwahi kukiongoza.
Tarehe 29 Mei, raia wa Afrika Kusini watapiga kura kuwachagua wajumbe 400 wa bunge, mwezi mmoja baadaye wabunge katika bunge jipya watachagua rais ajaye, huku wachambuzi wakisema upungufu wa wabunge utailazimisha ANC kutafuta washirika ili kusalia madarakani, suala ambalo litamfanya zuma kuwa turufu muhimu katika kinyang’anyiro cha kumchagua raia ajaye wa afrika kusini.