Na saulo Stephen – Singida.
Watuhumiwa 90 wa makosa mbalimbali, wamekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida, kufuatia operesheni maalum za kuimarisha ulinzi na usalama zilizofanyika katika maeneo tofauti ya mkoa huo.
Akizungumza na vyombo vya Habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, SACP Amon Kakwale amesema operesheni hizo zilianza mwezi Machi 2026 zikiwa na lengo la kukabiliana na vitendo vya uhalifu vinavyoathiri usalama wa raia na mali zao.
Katika operesheni hiyo, watuhumiwa 11 walikamatwa kwa kosa la mauaji, huku 24 wakikamatwa kwa tuhuma za kujeruhi. Aidha, watu 17 walinaswa wakijihusisha na biashara ya dawa za kulevya, ambapo mmoja alikutwa na lita 120 za mafuta ya dizeli yanayodhaniwa kuwa ya wizi, na wengine wanne walikutwa na nyara mbalimbali za uhalifu.

Aidha watuhumiwa wanne walikamatwa kwa tuhuma za kuvunja nyumba na kuiba mali, wakiwemo waliokutwa na vifaa kama runinga, redio, pasi za umeme na vifaa vya kilimo,huku Watuhumiwa wengine tisa wanashikiliwa kwa kuvunja nyumba usiku na kuiba mali zikiwemo godoro, fedha taslimu na vifaa vya umeme.
Katika hatua nyingine Kamanda Kakwale amebainisha kuwa watu 29 walikamatwa kwa makosa ya uzembe na uzururaji, huku mmoja akikutwa na silaha aina ya gobole bila kibali. Polisi pia walibaini matukio ya wizi wa mifugo na vipikipiki, na hatua za kisheria zinaendelea dhidi ya watuhumiwa.
Polisi wamewataka wananchi wa Singida kuendelea kutoa taarifa za uhalifu kwa wakati ili kusaidia juhudi za kudumisha amani na utulivu, wakisisitiza kuwa ushirikiano kati ya jamii na vyombo vya dola ni muhimu katika mapambano dhidi ya uhalifu.


