Na Gideon Gregory – Dodoma.
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Juma Homera amesema katika kipindi cha Julai, 2025 hadi Machi, 2026 Wakala wa usajili ufilisi na udhamini (RITA) umesajili na kutoa vyeti 468 vya talaka ikilinganishwa na vyeti 675 vilivyotolewa kipindi kama hicho katika mwaka 2024/2025.
Dkt. Homera ameyasema hayo leo Aprili 24,2026 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2026/27.
“Kutokana na takwimu za talaka natoa wito kwa viongozi wote waliopewa dhamana ya kufungisha ndoa, wazazi na walezi kuendelea kutoa elimu ya maadili kwa wanandoa, na kujenga utamaduni wa kuvumiliana na kutatua changamoto zinazojitokeza kwa njia ya majadiliano ili kupunguza talaka zinazo athiri malezi ya watoto kwa mustakabali wa haki zao na kusajili ndoa zilizovunjwa kwa amri ya Mahakama ili kulinda haki za kisheria,” amesema.

Katika hatua nyingine Dkt. Homera amesema RITA imesajili na kutoa vyeti 25 vya kuasili watoto ikilinganishwa na vyeti 29 vya kuasili watoto vilivyotolewa kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Kuhusu suala mirathi Waziri Dkt. Homera kipindi cha Julai, 2025 hadi Machi, 2026 Wakala ulipokea mirathi mipya 15 kutoka amri za Mahakama za kumwelekeza Kabidhi Wasii Mkuu kuwa msimamizi wa mirathi ikilinganishwa 14 iliyopokelewa kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha 2024/2025 na kufanya jumla ya mirathi inayosimamiwa kufikia 129.
“Katika kipindi husika mirathi moja (1) imefungwa baada ya kugawa mali kwa wanufaika na 128 inaendelea kufanyiwa kazi. Aidha, katika kipindi husika, Wakala umeandika na kutunza wosia 136 ikilinganishwa na wosia 109 zilizoandaliwa na kutunzwa kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 25,” amesema.
Homera ameongeza kuwa, Wakala unaendelea na maboresho ya kuimarisha uandishi, uhamasishaji na uhifadhi wa wosia ili kuondoa migogoro inayojitokeza katika usimamizi wa mirathi nchini.


