Saada Almasi – Meatu.
Mgombea wa nafasi ya Ubunge jimbo la Meatu kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Salum Khamis Salum ameendelea na ziara yake ya kuzinadi sera za chama cha Mapinduzi na kuomba kura kwa wanachi wa jimbo hilo kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025.
Akiwa kata ya Imalaseko amehutubia kijiji cha Isanga, Mwanhumbi, Kiloleli na Isebanda, amewahakikishia wananchi hao kuwa katika kipindi ambacho atapewa ridhaa ya kuongoza, atapambana na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama sambamba na kuendelea kupambana na Wanyama Tembo kwa kuhakikisha wanaondolewa katika makazi ya watu.

Akizungumzia suala la afya Salum amesema kuwa kwa sasa kuna maboresho makubwa ya sekta hiyo ambayo ni kipeumbele kwa kuhakikisha ujenzi wa zahanati zilizoishia njiani zinakamilika na kuanza kufanya kazi huku mpango wa kujenga zahanati katika kila kijiji na nyumba za waganga ukitekelezeka ndani ya miaka mitano ya uongozi wa chama hicho sambamba na kuongeza wataalamu wa kada hiyo ili kutoa huduma bora na zenye Utu wa Wananchi.
Akiwa katika kijiji ya Iramba ndogo, Mwangudo, Sungu na Makao ndani ya kata ya Mwangudo ameahidi maboresho ya vyumba vya madarasa na nyumba za walimu huku akitoa msisitizo wa kuongeza ushindani wa zao la pamba ili bei ya kilo moja ipande kutoka shilingi 1150 kwa sasa hadi kufikia 2000 kwa kilo moja.

“Mimi ujanja unaotumika ninaujua kuna gharama ambazo zinaongezwa katika usafirishaji na uchakataji ambazo zinakuja kumuathiri mkulima wa chini kwa hiyo ujanja ni kuhakikisha kila gharama inayopangwa na wanunuzi tunaiangalia na kuipigia hesabu upya ili kile kidogo kinachoongezeka katika bei ya mafuta na usafiri nk kirudishwe kwa mkulima wa chini ili bei ya kilo ipande,” amesema Salum.
“Na pia habari ya kuwa na mzabuni mmoja wa kuwapa mbegu madawa na baadae awe mnunuzi ndiyo inawaumiza zaidi kwa hiyo nitahakikisha kunakuwa na wanunuzi zaidi ya wanne nyie mtachagua muuze kwa nani na mchukue pembejeo kwa nani kufuatana na faida mtakazozipata,” ameongeza Salum.

Katika ziara hiyo pia amezungumzia suala la maboresho ya miundombinu ya mawasiliano ya barabara pamoja na kuondolewa kwa tozo katika barabara ya Meatu kwenda Arusha kupitia Makao ambayo imekuwa ikisababisha kuhama kwa magari katika njia hiyo.


