Na Ibrahim Rojala – Geita.
Viongozi wa dini na washiriki wao wametakiwa kuhakikisha wanaepukana na vitendo vya rushwa, haki za raia kutoingiliwa hususani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, kwa ni adui wa haki, kosa la kimaadili, kiimani na kosa la jinai kwa mujibu wa Sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa sura ya 329 na marejeo yake ya mwaka 2022.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Geita, Alex Mpemba Oktoba 2, 2025 wakati akizungumza katika kikao kazi cha Taasisi hiyo na viongozi wa dini kilichoketi kwa lengo la kutambua nafasi ya viongozi wa dini katika mapambano dhidi ya rushwa kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2025 akieleza kwamba viongozi hao wanapaswa kufikisha elimu ya mapambano dhidi ya rushwa kwa washirika.
“Kama mnavyofahamu ndugu viongozi wa dini rushwa ni adui wa haki, rushwa ni kosa la kimaadili, rushwa pia ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria zetu za Tanzania,sasa kwa upande wa kiimani, makosa ya kiimani yanakuwa na jina linguine, makosa ya kiimani yanaitwa dhambi, kwahiyo kwa maana hiyo rushwa ina kila sifa ya kuitwa dhambi,” amesema Mpemba.

Amebainisha kwamba moja kati ya majukumu ya TAKUKURU ni kuzuia vitendo vya rushwa kwa kushirikisha umma kwa njia ya elimu kama ilivyofanya kwa kuwashirikisha viongozi wa dini ambao nyuma yao wana waumini wengi ambao wanawasikiliza.
Amesema, mafunzo waliyoyapata ni muhimu sana kwani yalilenga kuwaongezea ujuzi na ufanisi wa kuelimisha jamii kuhusu ubaya wa rushwa na kuihamasisha jamii ili ishiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kuzuia kukemea na kutoa taarifa za vitendo vya rushwa.
Akiwasilisha mada katika kikao kazi hicho, Mwenyekiti mwenza wa kamati ya amani,viongozi wa dini mkoa wa Geita na Askofu wa Kanisa la TMRAC, Askofu Stephano Saguda amesema Mungu amewaweka binadamu duniani ili kumuwakilisha yeye na kuhakikisha wanatenda haki.

“Mungu anasema kwamba amewaweka muamue kwa haki, TAKUKURU mmepewa nafasi hii mumuwakilishe Mungu kwa haki,na kwa maana hiyo mnapaswa kusimamia kweli japo ni wakati mgumu unashawishika,mtu anakuletea burungutu la pesa ili wewe upindishe tu kwamba umruhusu yeye afanye ni kazi ngumu waheshimiwa,” amesema Askofu Saguda
Kadhi wa Mkoa wa Geita, Sheikh Ibun Badhi Rajab akizungumza kwa niaba ya Sheikh wa Mkoa wa Geita alisema wanaokula, kusambaza na kupokea rushwa ni Watanzania ambao pia ni waumini wa dini zilizopo nchini na hivyo kutoa wito kwa Viongozi wa Dini kueleza mmashara ya rushwa kwa Taifa.
“Rushwa haikubaliki katika Quran,rushwa haikubaliki katika Biblia na rushwa haikubaliki katika mazingira nan miongoni mwa matokeo yake ni laana inayokwenda kwa aliyetoa,aliyepokea na aliyesababisha tendo la rushwa kukamilika lakini pia inatia umaskini,kuleta chuki ndani ya jamii na taifa au nchi kukabiliwa na ukame,” amesema Sheikh Ibun.

Baadhi ya wajumbe walioshiriki katika kikao kazi hicho wamependekeza maazimioa mbalimbali kama vile uwepo wa somo maalum la rushwa katika shule kuanzia ngazi za chini, viongozi wa TAKUKURU kutembelea vijiwe vyenye mikusanyiko ya watu kwa lengo la kubaini vitendo vya rushwa katika wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu, nyumba za ibada kutotumika kama majukwaa ya siasa na viongozi wa dini kuwaacha washiriki wao kuamini katika itikadi za vyama walivyoamua kuvichagua kwa hiyari yao bila kuwaingilia na kuomba elimu ya rushwa kufikishwa vijijini.


