Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limeanzisha oparesheni maalum ya kuwakamata Majangili wanaohujumi mazao ya misitu ambapo limefanikiwa kuwakamata watu 25 kwa tuhuma za kukata mbao na kuchoma Mkaa kinyume na sheria.
Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita Kamishna Msaidizi wa Polisi Safia Jongo ambapo amesema oparesheni hiyo ilianza Oktoba 25 mwaka huu na Jeshi hilo limefanikiwa kukamata magunia ya Mkaa 410, vipande vya mbao 1965, pamoja na ng’ombe 406.
Kamanda Jongo amesema oparesheni hiyo inafanyika katika wilaya zote za mkoa wa Geita huku akisema jeshi hilo linatarajia kufungua kesi 16 mahakani za watuhumiwa hao ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria kama fundisho kwa wangine na kuwataka wanaoishi katika maeneo ya hifadhi za misitu kuhama mara moja.
Aidha Kamanda Jongo ameongeza kuwa oparesheni hiyo inakwenda sambamba na oparesheni ya Nyumba kwa nyumba kwa lengo la kuwasaka wahalifu mbalimbali wanaojificha majumbani kwa lengo la kutokomeza viashiria vyote vya uhalifu hasa kuelekea msimu wa sikukuu ili kuufanya Mkoa huo kuwa salama.
