RC DENDEGO AZITAKA TAASISI KUTOA MAFUNZO KWA WAANDISHI WA HABARI KUONGEZA UFANISI

Mkuu wa mkoa wa Singida, Halima Dendego ametoa wito kwa taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali kutoa mafunzo kwa wanachama wa klabu za waandishi wa Habari katika mikoa ili kuimarisha weledi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji na usambazaji wa Habari kwa umma. 

RC Dendego ametoa wito huo leo Januari 28, 2025 mkoani humo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wanachama wa klabu za waandishi wa habari wa mikoa ya Dodoma na Singida kuhusu matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 na tafiti nyingine za takwimu.

“Kufanya hivyo kutaongeza kutangazwa kwa shughuli nyingi zaidi za maendeleo zinazofanyika mikoani zikiwemo zinazofanywa na wananchi wenyewe kama kilimo, ufugaji, uvuvi na nyinginezo nyingi ambazo zinagusa maisha ya siku ya wananchi sio tu wa vijijini bali hata wanaoishi mijini,”amesema.

Amesema mafunzo hayo kwa wanachama wa Klabu za Waandishi wa Habari wa mikoa hiyo miwili yana umuhimu mkubwa kwa kuwa yanavijengea uwezo vyombo vya Habari katika kutafsiri, kufanya uchambuzi na namna ya matumizi ya matokeo ya Sensa na takwimu nyingine rasmi zinazozalishwa nchini. 

“Lengo la Serikali ni kuona matokeo ya Sensa na ya tafiti nyingine za kitakwimu yanawafikia wadau wote hususan wananchi ili waweze kuyatumia katika shughuli zao binafsi na pia kuzitumia katika kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi ikiwemo kushiriki katika kufanya maamuzi ikiwemo kupanga, kufuatilia na kutathmini shughuli za maendeleo zinazotekelezwa na Serikali na wadau wengine wa maendeleo katika maeneo yao wanayoishi,”amesema.

Kwa upande wake kamisaa wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, spika mstaafu Anne Makinda, amesema kuwa matarajio ya serikali baada ya mafunzo hayo ni washiriki kuwa wameongeza uwezo, ujuzi na weledi katika kuandika, kutangaza na kusambaza matokeo ya sensa pamoja na yale ya tafiti nyingine za takwimu zinazofanywa na NBS.

” Ni matarajio ya Serikali kuwa baada ya mafunzo haya ya siku mbili, washiriki watakuwa wameongeza uwezo, ujuzi na weledi katika kuandika, kutangaza na kusambaza matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi pamoja na matokeo ya tafiti nyingine za kitakwimu zinazofanywa na NBS,”amesema.

Pia ameongeza kuwa  katika kuhakikisha vyombo vya Habari vinakuwa na uelewa mpana kuhusu mfumo mzima wa uzalishaji na usambazaji wa takwimu, katika mafunzo hayo tumeandaa mada kuhusu tafsiri ya takwimu rasmi, misingi na vyanzo vyake, mada kuhusu mambo muhimu yanayozingatiwa katika uzalishaji wa takwimu rasmi yaani mfumo mzima wa kufanya tafiti za kitakwimu na mifumo ya usambazaji wa matokeo ya tafiti hizo.

” Tunafanya hivyo kwa sababu vyombo vya Habari ni mdau mkubwa katika kufanikisha 7 utekelezaji wa majukumu ya taasisi yetu ambayo ni kukusanya, kukuzalisha na kusambaza takwimu rasmi nchini,”ameongeza.

Kwa sasa Ofisi ya Taifa ya Takwimu ipo katika awamu ya tatu na ya mwisho ya utekelezaji wa sensa ya watu na makazi, ambapo awamu hii inajumuisha uchakataji, uchambuzi na uandishi wa ripoti ikiwa ni pamoja na usambazaji, kufanya mafunzo na kuhamasisha matumizi ya matokeo ya sensa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *