Wanafunzi saba wa Shule ya Sekondari Businda, Wilayani Bukombe, Mkoa wa Geita, wamefariki dunia na wengine 82 wamejeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bukombe, baada ya kupigwa na radi wakiwa Darasani.
Akizungumza na Wananchi Hospitalini hapo, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Paskas Muragili amesema Wanafunzi wawili wako kwenye hali mbaya na tulio hilo limeacha simanzi kwa jamii nzima.
Amesema, “tukio la ajali ya radi limesababisha vifo saba kwa Wanafunzi na kujeruhi wanafunzi 82 ambao wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali yetu ya wilaya.”
Kufuatia tukio hilo, Mbunge wa Jimbo la Bukombe ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa pole kwa wananchi wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita kufuatia ajali ya radi iliyotokea leo Januari 27, 2025 katika Kata ya Ushirombo.
Sehemu ya taarifa hiyo salamu za pole ya Dkt. Biteko iliyotolewa leo Januari 27, 2025 inaeleza kuwa ajali hiyo ya radi imesababisha vifo vya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Businda.
“ Nimepokea taarifa ya vifo vya watoto wetu wa Businda Sekondari kwa masikitiko makubwa. Naomba kuwapa pole sana wazazi, walezi, walimu, wanafunzi wa shule hii na ndugu wote waliguswa na msiba huu mkubwa,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa, “vifo vya vijana wetu vimetushtua sana wana Bukombe wote. Tunawaombea faraja familia zote zilizofikwa na msiba huu aidha, tunawaombea uponyaji wa haraka majeruhi wote kwenye kadhia hii.”
Aidha, Dkt. Biteko amemuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na Ofisi ya Mbunge kufuatilia kwa karibu matibabu ya majeruhi wote na taratibu za mazishi ya wanafunzi hao walioaga dunia.