Mzee wa miaka 99 Mkazi wa wilaya ya Mbogwe Mkoani Geita amefariki dunia kutokana na ugojwa wa kipindupindu huku wengine 11 waliobainika na ugojwa huo na kupatiwa matibabu wakiruhusiwa kurudi nyumbani katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela ameyasema hayo wakati akitoa taarifa ya ugojwa wa kipindupindu katika kikao cha kamati ya afya ya Msingi ya Mkoa ambapo amesema mpaka sasa Mkoa huo umebaini uwepo wa wagojwa 12 hali ambayo imepelekea mkoa huo kuanza kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi ili kukabiliana na mlipuko huo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Dr. Omary Sukari amesema mgojwa wa kwanza wa kipindupindu alibainika katika wilaya ya Mbogwe baada ya kufika katika kituo cha afya Masubwe akiwa na changamoto ya kutapika na kuharisha na baada ya kufanyiwa vipimo alibainika kuwa na ugojwa huo .